Kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa chama chake, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ametangaza kujiuzulu na kumaliza kipindi chake cha miaka tisa ya uongozi.

Trudeau amesema atakaa madarakani hadi Chama chake cha Liberal kiweze kuchagua kiongozi mpya, na bunge litaahirishwa – au kusimamishwa – hadi Machi 24.

“Nchi hii inastahili chaguo bora katika uchaguzi ujao na imedhihirika kwamba ikiwa nalazimika kupigana vita vya ndani, siwezi kuwa chaguo bora katika uchaguzi huo,” amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumatatu.

Trudeau aliingia madarakani mwaka 2015, akiwa na umri wa miaka 43 wakati huo, aliahidi aina mpya ya siasa inayozingatia sera za wazi juu ya uhamiaji, kuongeza kodi kwa matajiri na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.