Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
MAWAKILI wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoani Tabora wamelaani vikali kitendo cha kuzuiwa kutekeleza majukumu yake mmoja wa wanachama wake alipokuwa akifuatilia masuala ya wateja wake waliokamatwa.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana kwa niaba ya Mawakili wa Mkoa huo, Mwenyekiti wa TLS .koani hapa Wakili Kelvin Kayaga ameeleza kusikitishwa sana na kitendo hicho kilichofanywa na Jeshi la Polisi na Takukuru.
Amebainisha kuwa mnamo Januari 3 mwaka huu mwanachama wao Wakili Kilingo Hassan alipokea taarifa kutoka kwa wateja wake juu ya ndugu yao aliyekamatwa na kushikiliwa na Polisi hivyo akachukua hatua ya kufuatilia kwa Mamlaka husika.
Amefafanua kuwa licha ya kufuata taratibu zote kufuatilia suala hilo hakupewa ushirikiano wowote na alizuiwa kuonana na wateja wake huku wengine wakiruhusiwa kuonana nao na hata alipoenda Takukuru hakupewa ushirikiano.
Wakili Kayanga ameongeza kuwa licha ya Afisa wa Takukuru kuahidi kumweleza tuhuma zinazowakabili wateja wake aliporudi hakupata ushirikiano wowote hivyo akaamua kuandaa maombi kwa Mahakama ili Mamlaka hizo ziwafikishe mahakamani.
Baada ya kuwasilisha maombi hayo Wakili Kilingo alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa rumande na hata Viongozi wa TLS walipopata taarifa na kufika Kituoni hapo ili kumwombea dhamana walimyimwa.
‘Tunalaani sana kitendo hiki kilichofanywa na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) cha kumzuia Wakili Kilingo kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama Afisa wa Mahakama’, amesema.
Aidha tunalaani hatua ya Jeshi la Polisi na Takukuru kumkamata, kumshikilia na kumnyima dhamana ikiwemo kumnyang’anya simu yake kwa kosa ambalo kisheria linadhaminika, kitendo hicho kimesikitisha sana’, alisema.
Wakili Kayaga amebainisha kuwa Mawakili wote wa TLS Kanda ya Tabora pia wamesikitishwa sana na Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa jinsi walivyolipokea suala hilo na kushindwa kuwapa ushirikiano unaotakiwa.
Ameeleza kuwa katika kikao chao cha Januari 4, wameazimia kutoshiriki shughuli za Wiki ya Sheria mwaka 2025 ili kutuma ujumbe kwa Uongozi wa Mahakama na kutoshiriki kusimamia mashauri ya msaada wa kisheria kwa kipindi cha miezi 6 hadi hapo hatua zingine zitakapochukuliwa na Mamlaka husika.