Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
WATAALAMU wa Lishe katika halmashauri ya Wilaya ya Igunga Mkoani hapa wametakiwa kuongeza ubunifu utakaoleta matokeo chanya miongoni mwa jamii ikiwemo kuboreshwa afya zao.
Rai hiyo imetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya hiyo Sauda Mtondoo alipokuwa akifungua Kikao cha Wajumbe wa Kamati ya Lishe Wilayani humo ambacho pia kilikuwa na jukumu na kujadili bajeti ya kufanikisha majukumu yao.
Sauda amesisitiza kuwa Kamati hiyo ni muhimu sana kwa kuwa imebeba maslahi ya afya za wakazi wa Wilaya hiyo, hivyo akaelekeza Wajumbe wa Kamati hiyo kuja na mikakati chanya na inayotekelezeka kwa manufaa ya wananchi.
Amebainisha kuwa moja ya mikakati ya halmashauri hiyo ni kuongeza uzalishaji wa chakula lishe ili kujenga afya za wananchi na kupunguza tatizo la utapiamlo na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe.
‘Kikao hiki ni muhimu sana kwa kuwa kinajadili maslahi mapana ya jamii na afya zao, naamini bajeti itakayopitishwa itazingatia malengo ya halmashauri ya kuimarishwa suala zima la lishe miongoni mwa jamii, amesema.
Amefafanua kuwa huwezi kuzungumzia suala la uchumi au maendeleeo kama afya za wananchi haziko vizuri, na kubainisha kuwa afya inaanzia kwenye lishe bora.
Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa lishe bora ni tiba kwa magonjwa mbalimbali, hivyo anatamani Wilaya hiyo iwe na jamii yenye afya bora ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi vizuri na kujiongezea kipato.
Hatua hii itasaidia kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo akatoa wito kwa Wataalamu hao kuongeza ubunifu utakaoleta tija na matokeo chanya miongoni mwao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Joseph Mafuru ameshauri Wataalamu hao kuangalia uwezekano wa kutumia maeneo ya wazi yaliyo karibu na shule kuanzisha kilimo cha mazao lishe ikiwemo bustani za mbogamboga.
‘Maafisa Elimu tusaidieni kubainisha maeneo yaliyo wazi karibu na shule ambayo yanafaa kuanzisha bustani za mboga mboga na mazao mengine ili kuwezesha watoto wetu kupata chakula shuleni, ameeleza.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika halmashauri hiyo, Lucia Kafumu ameshauri Maafisa Lishe kuanzisha bustani za mboga mboga na mazao lishe mengine, kuuza maziwa na kufuga kuku.
Aidha amewataka kuboresha mipango yao ili kuhakikisha changamoto za lishe zinazoikabili jamii katika Wilaya hiyo zinatatuliwa na kuleta mafanikio chanya.