Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Leo naandika makala hii si kwa jambo jingine, bali kupanua wigo wa mjadala na kuwapa Watanzania muktadha wa siasa za kuanzia kwenye vyama na hatimaye kuingia Ikulu.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametangaza nia ya kugombea tena nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, baada ya kushika wadhifa huo kwa miaka 20.
Sitanii, niseme kwa mara nyingine Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepata fursa ya kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwapa Watanzania wa kada mbalimbali fursa ya kuzungumza na Watanzania bila upendeleo wala uonevu. Ni jukumu la wahariri katika nchi mbalimbali duniani kuandaa mikutano ya kihabari na viongozi, taasisi na mashirika mbalimbali kwa nia ya kuwapa fursa ya kuzungumza na wananchi.
Katika nchi zilizoendelea, hili halimshangazi yeyote. Hata hapa Tanzania lilikuwapo, kwani nakumbuka miaka ya nyuma Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akitaka kuwasiliana na Watanzania au kuzungumza jambo zito, aliwaita waandishi na wahariri kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam na leo tunazo hotuba zake nyingi zilizopatikana kupitia mikutano hii.
Hapa katikati utaratibu huu ulipotea. Ikawa watu wanatafuta jinsi ya kuzungumza na vyombo vya habari hawapati taasisi ya kihabari ya kuwaandalia mikutano hii wazungumze na wananchi.
Tangu mwaka 2021 nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), nikasema nitarejesha utamaduni wa Jukwaa la Wahariri kutoa nafasi kwa viongoza kuzungumza na wananchi kupitia TEF.
Sitanii, nafurahi hadi sasa Jukwaa la Wahariri katika mpango huu wa kuwaandalia viongozi mikutano, limefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Limeandaa mikutano mingi. Kati ya mikutano hii ni ule wa Juni 28, 2021 uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na wahariri. Mwingine ni huu uliofanyika Rio de Janeiro, ambapo Rais Samia pia alizungumza na wahariri wakiwa Brazil, akaeleza kuhusu manufaa makubwa ambayo nchi yetu imeyapata kwa kushiriki mkutano wa G20.
Si Rais Samia pekee, TEF imepata kuandaa mkutano na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ukafanyika makao makuu ya CCM. Katika mwendelezo huo, TEF imeandaa mikutano ya watu mashuhuri wengi, ila itoshe tu kumtaja Waziri Mkuu (mstaafu), Jaji Joseph Sinde Warioba uliofanyika mwezi uliopita. Ni katika mwendelezo huo, wiki iliyopita TEF imeandaa mkutano wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freema Mbowe.
Julai 14, 2023 TEF iliandaa mkutano uliohusu DP World, ambapo Mwanasheria Mkuu wa sasa, Hamza Johari, alitoa ufafanuzi wa kina juu ya mkataba wa DP World na Bandari, Watanzania wakaujua ukweli badala ya upotoshaji uliokuwa umetamalaki. Narudia, TEF tutaendelea kuandaa mikutano ya aina hii kwa nia ileile ya kuwawezesha Watanzania kufahamu ukweli badala ya kuacha uvumi wa mitandaoni. Hii ni sehemu ya kazi yetu kama wahariri.
Sitanii, nimepata mshangao kusoma katika mitandao ya kijamii na kumsikia Padri Wilbrod Slaa (ambaye kimsingi aliuacha huu wito na kujiunga na wito wa ndoa), akinishambulia kwa kumwandalia Mbowe mkutano huu. Inawezekana hakufahamu kazi ya wahariri, hivyo nadhani kwa kumtajia baadhi ya mikutano tuliyokwisha kuiandaa, naamini atafahamu kuwa kumbe hatukukosea kumwandalia Mbowe mkutano huo.
Mbowe amezungumza mengi katika mkutano huo. Amezungumza faida ya kiongozi kuwa na maridhiano, na kiongozi yeyote kuwa tayari kutumia mbinu mbalimbali katika uongozi, ikiwamo diplomasia na mabavu inapobidi. Ameeleza mafanikio aliyopata, ikiwamo moja ambalo wakati anaichukua CHADEMA mwaka 2003, ilikuwa na wabunge wasiozidi watatu wa kuchaguliwa , lakini mwaka 2005 ilifikia kilele kwa kuwa na wabunge 72.
Ameeleza mazingira ya kisasa yalivyobadilika kwa Rais John Pombe Magufuli kupiga marufuku shughuli za kisiasa nchini, katazo lililoendelea kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2023 lilipoondolewa na Rais Samia Suluhu Hassan. Mbowe aligusia kuwa mwaka 2020 katika uchaguzi, CCM walipita bila kupingwa, hivyo CHADEMA ikapoteza wabunge wote ikabaki na wabunge sifuri.
Kimsingi ameeeleza vema kuwa katika kipindi hicho cha miaka saba ni wazi chama kilikufa kifo cha asili. Ni katika kipindi cha mwaka mmoja, baada ya siasa kuruhusiwa kwa maana ya 2023 na 2024 ndipo shughuli za kisiasa zimerejea. Shughuli za kisiasa zimekuja na maridhiano. Zimefutwa kesi za kisiasa zaidi ya 400, zikiwamo za watu waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Rais Samia ameruhusu waliokuwa wakimbizi wa kisiasa kurejea nchini, ambapo Tundu Lissu, Godbless Lema, Ezekia Wenje na wengine wamerejea kutoka uhamishoni na wakaanza kufanya siasa bila vikwazo. Si hilo tu, CHADEMA ilikuwa kimesusa kupokea fedha za ruzuku kwa kutotambua matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020. Kupitia maridhiano, wamekubali kupokea ruzuku.
Ruzuku ya vyama vya siasa inatolewa kwa utaratibu wa idadi ya kura za ubunge kwa asilimia 50 na idadi ya wabunge walioshinda kwa asilimia 50. Hivyo pamoja na CHADEMA kuwakataa wale wabunge 19, bado wanayo sifa ya kupokea ruzuku inayotokana na kura walizopata zilizovuka asilimia 5 ya kura za ubunge kote nchini. Hii maana yake si kwamba kupata ruzuku lazima uwe na wabunge, la hasha, bali ufikishe angalau asilimia 5 ya kura za ubunge zikijumulishwa kura zote nchini baada ya uchaguzi.
Uamuzi huu, umewapatia CHADEMA Sh bilioni 2.6 kwa mkupuo, ambazo wametumia sehemu ya fedha hizo kununua jengo la ofisi ya kudumu pale Mikocheni, Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 1.6. Mbowe ametaja mengi katika maridhiano na akahoji, ikiwa hayo ni mambo mabaya kuyafikia kwenye maridhiano, basi mshindani wake ambaye ni Makamu Mwenyekiti wake Lissu, aeleze lililo jema ni lipi kwa chama chao na nchi.
Sitanii, binafsi nimefuatilia siasa za ujenzi wa vyama vya siasa na ukombozi wa nchi zetu. Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni mrithi wa TANU na ASP vilivyoungana mwaka 1977. Mwalimu Julius Nyerere alikiongoza chama hiki kwa miaka 36 kuanzia mwaka 1954 hadi 1990 alipong’atuka. Muda huu ulimsaidia kujenga falsafa ya chama, kujenga mifumo na kuandaa viongozi.
Nitaje viongozi wachache waliojenga vyama hadi wakafanikiwa kuwa marais, lakini baada ya kushika madaraka ya dola (urais), ajenda ya ukomo wa uongozi ikachukua mkondo. Rais Kenneth Kaunda wa Zambia ameongoza UNIP tangu mwaka 1960 hadi mwaka 1991 alipotoka madarakani.
Rais wa kwanza wa Marekani, George Washington aliongoza Jeshi la Mapinduzi ya Kikatiba tangu mwaka 1775, akafanikiwa kuandika Katiba ya Marekani mwaka 1776, miaka 14 baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Marekani, yaani 1789.
Washington aliongoza taifa hilo kwa miaka minane kuanzia 1789 hadi mwaka 1797 alipostaafu. Yaani aliongoza miaka 21 tangu ameanza harakati za kisiasa. Sitamtaja Malkia wa Uingereza, Elizabeth. Nimeona nitaje mifano michache, kwani kwa vyama vya ukombozi kwa nchi za Afrika na duniani ni mingi. Nyakati nyingine hivi vyama vya upinzani, vinahitaji mtu anayevifahamu. Mtu anayeiishi falsafa ya chama husika na kukijenga hadi kinaaminika kwa wapiga kura.
Sitanii, wakati nahitimisha makala hii naomba ifahamike kuwa katika ngazi ya nchi, ikiwa mtu anachaguliwa kuwa Rais wa nchi, basi ni vema tukaheshimu ukomo wa vipindi viwili, lakini huko kwenye vyama, ikiwa wanachama wanamwamini mwenyekiti wao na wanaona anakubalika, wanayo nafasi ya kumwondoa kwa njia ya kura hata baada ya kipindi kimoja au kuendelea kumchagua hadi afanikishe malengo yao ya kuingia Ikulu. Ikifika Ikulu, ajue Kanuni ya Vipindi Viwili inamhusu. Ndiyo maana nasema CHADEMA hawana sababu ya kukashfiana, ikiwa Lissu anakubalika zaidi ya Mbowe, Januari 23, 2024 ni wazi wapiga kura wataamua.
Kwa vyovyote vile iwavyo, naomba ifahamike kuwa utamaduni wa siasa za Tanzania ni tofauti mno na siasa za majirani zetu. Sisi hata uhuru wetu haukupatikana kwa watu kwenda msituni au kutumia vurugu. Siasa za hoja kwa hoja ndiyo nguzo ya utulivu na amani ya Tanzania. Mbowe amesema anaamini katika siasa hizo, ikiwa wana CHADEMA wanaamini katika matumizi ya nguvu, basi watamchagua huyo anayehamasisha hilo. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827