Na Joseph Mihangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

“Yuko wapi yeye aliyezaliwa, Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki na tumekuja kumsujudia.”
Haya ni maneno ya Mamajusi (wenye busara) wa Mashariki waliofika Yerusalemu kwa ajili ya kumsujudia na kumpa zawadi mtoto Yesu. Alizaliwa na mama Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu takriban miaka 2025 iliyopita kama inavyoelezwa katika Biblia Takatifu, Injili ya Matayo 2:2.

Neno ‘Mfalme wa Wayahudi’ lilimghafilisha na kumtia hofu mtawala wa nchi hiyo, Mfalme Herode, akiona uwezekano wa kupokonywa utawala na mzaliwa mpya akikua kama ilivyotabiliwa na manabii.

Tukio hili muhimu lilitabiriwa kwa uthabiti na Nabii Isaya miaka 700 kabla ya kuzaliwa Kristo kwa maneno yafuatayo:

“Tazama, bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto mwanaume naye atamwita jina lake Imanueli.” Isaya 7:14.
Tena ikatabiriwa watu wa kwanza kutoka mbali watakaomuona mahali alipozaliwa kwamba:
“… wakati huo BWANA wa Majeshi ataletewa Hedaya (zawadi) na watu warefu, laini; watu watishao tangu mwanzo hata sasa; taifa la wenye nguvu wakanyagao watu, ambao mito inakata nchi yao (Kushi); mpaka mahali pa jina la BWANA wa Majeshi, Mlima Sayuni.”

Kwa hofu hiyo, na ili kuzuia hilo lisitokee, Mfalme Herode alituma watu (askari wake) kwenda kusaka na kuwaua watoto wote wanaume huko Bethlehemu na viunga vyake, kuanzia watoto wenye miaka miwili na chini ya hapo, mlengwa mkuu akiwa Kristo ambaye mpaka hapo ilikuwa haijulikani lini na wapi alipozaliwa katika kipindi cha miaka miwili kurudi nyuma.

Usiku, Malaika wa Bwana akamtokea Yusufu, mumewe Maria katika ndoto, akamwambia yeye, mama na mtoto wakimbilie Misri kumwepusha mtoto Yesu asiuawe, na wakae huko hadi kifo cha Herode.

Haielezwi eneo gani na kwa muda gani walikaa Misri na njia waliyotumia kutoka na kurejea Bethlehemu.
Kuna maswali yenye kuhitaji majibu hapa: Bethlehemu au Nazareth ya kipindi hicho ilikuwa bara gani na ilikaliwa na kutawaliwa na watu gani?

Mamajusi walikuwa kina nani na kutoka Mashariki ya wapi? Watu warefu wenye nguvu kwa mujibu wa utabiri wa Nabii Isaya ni kina nani? Kwa nini Kristo alitoroshewa Afrika na si Palestina?

Kabla ya kupata majibu, ni vema tuweke vema historia kwanza: kwamba, kipindi cha Kristo, Bethlehemu, Palestina, ilikuwa sehemu ya Afrika Mashariki ya Kaskazini.

Neno au nchi ya ‘Mashariki ya Kati’ haikuwapo hadi miaka ya 1850 kufuatia kujengwa na Waingereza kwa mkondo – bahari unaofahamika kama ‘Suez Canal’ miaka mingi baada ya Kristo.

Licha ya ukweli juu ya sehemu takatifu alikozaliwa, kuna ushahidi tele katika Biblia kuonyesha kwamba, Kristo hakuwa mtu mweupe kama inavyoelezewa leo, bali mtu mweusi, yeye na ukoo wake.

Rahabu, Tamari, Makeda au kwa jina jingine ‘Malkia wa Sheba’, Mfalme Suleiman, Batsheba na wengine, wote walikuwa watu weusi.

Abrahamu pia, ambaye ndiye baba wa Ukristo na Uislamu (Watu wa Kitabu) alizaliwa kwenye mji wa mtu mweusi, Nimrod, mwana wa Kushi.

Katika Kitabu cha ‘Wimbo wa Suleiman’, Mfalme huyo anajisifia kwa kusema: “Mimi ni (mtu) mweusi lakini (mtanashati) wa kupendeza.”

Tusisahau pia kuwa Kristo alipotoroshewa Misri ili asiuawe na Herode, alipelekwa kufichwa huko miongoni mwa Waafrika Weusi asitambulike kuliko kama angefichwa miongoni mwa watu weupe.
Kipindi hicho Misri ilikuwa chini ya utawala wa Kirumi.

Kutoka Ethiopia ya kale hadi Urusi, sanamu za Kristo za kwanza zilizoenea zilimwonyesha kama mtu mweusi.
Kabla ya kipindi cha ‘Mvuvumo wa Ulaya’ (European Renaissance) karne ya 16, Kristo alifahamika kama mtu mweusi sawa na watu wa maeneo yake.

Sanamu zote za kidini, kuanzia Yosefu, Maria na mitume wote zilichongwa au kuchorwa kwa sura na rangi ya mtu mweusi. Ni kipindi cha ukoloni ambapo sura ya Kristro ilianza kuonyeshwa kama mtu mweupe.

Mwaka 1561, Papa Alexander wa VI wa Rumi, alimwajiri mchoraji – mchongaji sanamu mahiri, Leonardo Da Vinci, kuchora/kuchonga sanamu ya Kristo kwa sura ya mwanaye kwa (mama kimada), Ceasar Borgia na kuitangaza kuwa ndiyo sura pekee ya kutumika kwa makanisa yote kwa Imani ya Kikristo.

Picha hiyo ilifanyiwa maboresho zaidi mwaka 1938 na mchoraji wa Kimarekani, Salman Warner, kuwa ya mwonekano wa Kristo wa Kimarekani na ambayo ndiyo inayotumika duniani kote hadi sasa.

Mtu mweusi alikalia na kutawala Palestina kwa maelfu ya miaka, kikiwamo kipindi ambacho kilihesabiwa kama sehemu ya Afrika.

Hii yote ilijulikana kama nchi ya Kushi, Ethiopia, Nubia au Misri. Kushi ilitawala nchi zote za sasa za Maziwa Makuu, Ethiopia, Misri, Jordan, Lebanon, Israel, Saudi–Arabia, Sudan, Iran na Mesopotamia ambayo sasa inaitwa Iraq.

Mmoja wa watawala mahiri wa himaya ya Kushi aliyezitisha na kuzitetemesha nchi hizi, ni Farao Tirhakah, aliyetawala kati ya mwaka 690 na 664 Kabla ya Kristo (KK).

Ethiopia ni neno linalotokana na Kiyunani ‘Aithiops’, kumaanisha ngozi iliyoungua kwa jua (Matendo ya Mitume 8:27) likimaanisha watu weusi kutoka Ufalme wa Kushi.

Mbali na jina hilo, Kushi inajulikana pia kwa majina tofauti kama vile Nubia (Sudan), na Ethiopia enzi za zama za kale (Jeremia 36:14).

Kama Mfalme Nimrod, mtoto wa pili wa Kushi alitawala Mesopotamia (Iraq) kati ya mwaka 690 – 664 KK na kabla ya babu wa imani wa Wakristo na Waislamu, Abraham, aliyeishi mji wa Ur, kwa nini nchi hiyo isiitwe ya watu weusi kwa asili?

Nimrod anaitwa mpiganaji shujaa na mwindaji hodari wa kwanza duniani (Mwanzo 10:8-12).
Ukoo wa Abrahamu ulisambaa kutoka Sudan/Nubia hadi Ethiopia na baadaye kuvuka Bahari Nyekundu (Red Sea) hadi ukanda wa Arabia Kusini na kuingia Mesopotamia Kaskazini na kufanya makazi kati ya mwaka 4000 na 3000 KK.

Terah, baba yake Abrahamu aliyekuwa pia mtawala – mhubiri wa dini ya Kiafrika (Theolojia ya Kikemeti) ya ‘Horus’ au ‘Heru’, familia yake ilihama kutoka Edfu, Nubia hadi Mesopotamia na kufanya makazi Ur – Kasdim, maili chache kusini mwa Uruk.

Theolojia ya Kikemeti ilikuwa ya kwanza duniani kuamini Mungu mmoja, Utatu Mtakatifu (Mungu Baba, Mungu Mwana – Horus, na Mungu Mama – Isis), ambayo Mtaguso wa Kwanza wa Nicae wa mwaka 325 BK ulifuta nafasi hiyo na kuingiza nafasi ya Roho Mtakatifu; kuunda Utatu Mtakatifu mpya.

Kutoka Theolojia ya Kikemeti, Ukristo umeazima na kuridhia mengi zaidi ya asilimia 70 ya mafundisho yake.
Hajir, mama wa Kiafrika kutoka Nubia na mke wa pili wa Abrahamu, ni mama wa Nabii Ishmael.

Kwa sababu hiyo, ni bibi wa Waislamu wote kwa kuwa Mtume Muhamad (S.W.A) ni wa ukoo wa Ishmael. Kwa hiyo ni bibi wa Waarabu wote pia.

Wakemeti walioana kiukoo kwa hofu ya kuchanganya mbegu na kupoteza ukoo. Abrahamu alimuoa Sarah, mama yake Isaka, na baadaye akamuoa Keturah, kisha Hajir, mama wa Ishmael.

Kina mama wote hao walikuwa Wakushi kutoka Nubia na waumini wa dini ya Kiafrika ya Horus (Horites).
Na kama tutakavyoona baadaye, baba wa Nabii Musa, Mzee Amrani, alioa wake wawili wa Kikushi, Jacqueth au Jochbed, mama wa Musa, Harun na Miriam.

Na mke mwingine Ishar, mama wa Korah na Harun. Wawili hawa Korah na Harun ndio walioongoza maasi/mgomo Jangwani dhidi ya Musa kuelekea Kaanani.

BETHLEHEM, WEST BANK – DECEMBER 24: Palestinian marching band parade as part of Christmas celebrations in Bethlehem, West Bank on December 24, 2020. ( Issam Rimawi – Anadolu Agency )

Wote walikuwa wahubiri wa Theolojia ya Kikemeti kabla ya kuzuka kwa dini ya Uyuda (Judaism).
Nabii Musa alioa wake wawili wa Kikushi/Kinubi, kama alivyokuwa yeye. Wa kwanza aliitwa Tharbis na wa pili, Ziporah, binti wa mhubiri wa Midian na mshauri wa zamani wa Farao, Yethro wa ukoo wa Abrahamu kwa mke wa pili, Keturah.

Kufikia hapo tunaona kwamba, kuanzia Kushi baba wa Mfalme Nimrod, Abrahamu na uzao wake wote walikuwa wa asili ya Kushi/Nubia kama watu weusi wa imani ya Kikemeti (Mwanzo 2:11).

Hawa ndio waliomtambua Kristo kama mbegu ya mwanamke iliyoahidiwa (Mwanzo 3:15).
Mwanamke huyo ndiye Bikira Maria (Luka 1:35); kifo na kufufuka kwa Kristo siku ya tatu yalikuwa matarajio yao.

Mamajusi ni kina nani?

Nyota iliyowaongoza Mamajusi hadi alikozaliwa Kristo inajulikana kama ‘Nyota ya Wenye Busara’. Hawa walikuwa wanajimu mahiri wenye nguvu kutoka Kushi.

Walivukia Jangwa wakitokea Kusini Mashariki ilivyotabiriwa na Nabii Balaam (Hesabu 24:17). Walikuwa Waafrika kutoka Kushi.

Nyota iliyowaongoza Mamajusi hao ilimeremeta kwa rangi sita kuwakilisha watoto sita wa Kushi (Wajukuu wa Ham) ambao ni Seba, Havillah, Sautah, Raamah, Sabtecha na Nimrod kuonyesha kwamba yote yaliyokuwa yakitendeka yaliwakilisha theolojia na utamaduni wa Kiafrika (Mwanzo 5:32; 10:6–18).

Mamajusi wameelezewa kama watenda miujiza, watabiri mahiri (Danieli 2:2), wenye akili mara kumi zaidi ya wachawi na wataalamu wa nyota wote duniani. Wote walitoka Kushi kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya (Isaya 18:7).
Utawala wa mtu mweusi ulianza miaka 5,900 baada ya anguko la Adam huko Eden. Bustani ya Eden ilikuwa katika nchi ya Kushi ambayo sasa ndiyo Afrika Mashariki ya Maziwa Makuu.

Nchi walizotawala wana wa Ham, ikiwamo Palestina zimeelezewa vema kwenye maandiko, Yeremia 46:9; na nguvu yao kidunia (Yer. 46:9; Ezek. 30:5; Mwz. 10:5; Zab. 78:51; 105:23;106:22).
Ukuu, nguvu na utukufu wa Mwafrika umeelezewa vizuri tangu zama za kale na Nabii Isaya (Isay. 18:1,2,7; na Mwanzo. 10:8–10).

Kama Abrahamu ni wa uzao wa Nimrod, Mkushi mweusi aliitwa na Mungu kutoka Mesopotamia, Yesu Kristo aliitwa na Mungu kutoka Afrika/Kushi kwa kazi ya ukombozi.

Kwa mantiki hiyo, historia ya Mwafrika ni historia ya ukombozi wa dunia.
Hakuna popote kwenye Agano la Kale anapotajwa mtu mweupe kwa shughuli ya ukombozi.

Ameanza kutajwa kuanzia Agano Jipya kwa nahau na mfumo wa ukoloni na ubeberu wa kiroho, kiuchumi na kiutamaduni na kwa kufifisha Injili asilia ya Kristo na ukombozi wa kweli.

Katika makala inayofuata, tutaona njia waliyopita Maria, Yosefu na mtoto Yesu kwenda na kurejea kutoka Misri/Kushi, mahali walipoishi na masaibu waliyokumbana nayo.

Tutaona pia sababu za Afrika kuwa ya kwanza kupokea na kueneza dini ya Kiyuda/Kikristo kabla ya Ulaya Kaskazini, moja ya sababu hizo ikiwa kushabihiana kwa sehemu kubwa kati ya Ukristo na Theolojia ya Kikemeti.

Ni kwa kiwango gani maandiko ya Biblia ya leo yanashabihiana na Injili asilia ya Kristo, manabii na mitume kwa usahihi, kimantiki, maudhui na kwa njia ya uzima na kweli?
Nini kimetokea tangu Mtaguso wa Nicaea wa mwaka 325 BK kuhusu Injili ya kweli?

Itaendelea…