Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
VIONGOZI na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora wametembelea familia ya mjane wa Kada wa CCM Jastin Magembe aliyejiua kwa sumu baada ya mgombea wao kushindwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katibu wa CCM Mkoa Komredi Wilson Nkambaku na Wajumbe wa Sekretarieti ya Chama Mkoa wamefika nyumbani kwa marehemu katika Kitongoji cha Ikomwa Mlimani, Kata ya Ikomwa, Manispaa ya Tabora ili kumfariji Kada huyo aliyekuwa Kampeni Meneja wa mgombea na Mjumbe wa Baraza la UVCCM katani hapo.
Akitoa salamu za pole kwa wafiwa na wanaCCM wote katika Kata hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Balozi Dkt Emanuel Nchimbi, Komredi Nkambaku ameeleza kuwa chama kimepokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo la kujiua kada wao.
Amebainisha kuwa marehemu alikuwa mwanachama mahiri aliyesimamia vema shughuli za chama na alitoa mchango mkubwa kwa chama na kwenye kampeni za uchaguzi huo uliomalizika hivi karibuni ambapo mgombea wa CCM alishindwa.
Amewahikikishia wanafamilia kuwa CCM itaendelea kumuenzi kada wake aliyetangulia mbele za haki kutokana na mchango mkubwa aliotoa katika kupigania maslahi ya chama chake na wataendelea kuwa karibu na familia hiyo.
Nkambaku amewasihi wanaCCM na jamii kwa ujumla kuendelea kukiamini Chama chao na kubainisha kuwa hata kama wamepoteza kiti hicho serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan haitaacha kuwaletea maendeleo.
‘Kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali yenu ya CCM, naamini Kitongoji hiki kitarejea kwenye himaya ya CCM, kuweni na amani, tabasamu yenu itarudi kama ilivyokuwa huko nyuma’, ameeleza.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa huo, Komredi Iddi Moshi Mambo, ameeleza kuwa marehemu Jastin Magembe John ni askari mtiifu wa Chama aliyefia vitani hivyo Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kumkumbuka daima kama shujaa wake.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikomwa kwa awamu 2 mfululizo, Magembe John Spemba ambaye ni baba mzazi wa marehemu amewashukuru sana Viongozi hao kwa kwenda kuwafariji na kuahidi kuwa wataendelea kukitumikia Chama chao.
Akifafanua zaidi Katibu wa CCM wa Kata hiyo Gabriel Richard Maige amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 28 mwaka huu siku 1 tu baada ya kumalizika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo mgombea wao alishindwa.