Chombo hicho cha Parker Solar Probe kilisafiri katika angahewa ya nje ya nyota yetu, kikistahimili joto na mionzi mikali.
Hakitakuwa na mawasiliano yoyote kwa siku kadhaa wakati huu wa joto kali na wanasayansi watakuwa wakisubiri ishara, inayotarajiwa tarehe 27 Desemba, kuona ikiwa kimenusurika.
lengo ni kwamba uchunguzi unaweza kutusaidia kuelewa vyema jinsi Jua linavyofanya kazi.
Dkt Nicola Fox, mkuu wa sayansi katika Nasa, aliiambia BBC News: “Kwa karne nyingi, watu wamejifunza kuhusu Jua, lakini hupati uzoefu wa mazingira ya mahali hadi utakapotembelea.
“Na kwa hivyo hatuwezi kuona anga ya nyota yetu isipokuwa iwapo tutaipitia.”
Chombo hicho cha Parker Solar Probe kilizinduliwa mwaka wa 2018, kuelekea katikati mwa Mfumo wetu wa Jua.
Tayari kimepita karibu na Jua mara 21, ikikaribia zaidi, lakini ziara ya Mkesha wa Krismasi ni ya kuvunja rekodi.
Kwa kukaribia kwake, chombo hicho kiko umbali wa maili milioni 3.8 (kilomita milioni 6.2) kutoka kwenye uso wa jua
Hii inaweza isionekane kuwa karibu, lakini Nicola Fox wa Nasa anaelezea katika mtazamo wake: “Tuko maili milioni 93 kutoka kwa Jua, kwa hivyo nikiweka Jua na Dunia umbali wa mita moja, Parker Solar Probe iko sentimita nne kutoka kwa Jua – kwa hivyo hiyo ni karibu.”
Uchunguzi utalazimika kustahimili halijoto ya 1,400C na mionzi ambayo inaweza kuharibu nyaya za ndani za chombo hicho.