RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuungamkono juhudi za Muhimili wa Mahkama zenye lengo la kuleta mageuzi makubwa katika miundombinu ya majengo ya Mahakama.
Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa MahAkama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza, Serikali imefanikiwa kuleta mageuzi makubwa kwenye majengo ya Mahkama kwa kutoa fedha za ndani kwa asilimia mia jambo alilolieleza kuwa la kujivunia.
Aidha amesema mageuzi hayo yana lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi katika mazingira yakuridhisha hatua aliyoielezea kwamba itaijengea heshima muhimili huo.
“Tumetumia fedha zetu wenyewe kwasababu tungetumia wafadhili tungechelewa kufikia mafanikio haya” amebainisha Rais Dk Mwinyi.
Akilizungumzia jengo la zamani la Mahakama ya Vuga, Rais Dk. Mwinyi ameeleza litaendelea kuwa la Mahakama na kuridhia azma ya Mahakama ya kulifanya jengo hilo kuwa makumbusho ya Mahakama.