a Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametangaza kuwa Januari, 2025 utafanyika uzinduzi mkubwa Kariakoo wa biashara Kufanyika masaa 24.

Chalamila ameyasema hayo leo Desemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya.

Amesema serikali imeanza kuboresha miundombinu ya Kariakoo, ikiwa ni pamoja na kuweka kamera za usalama, taa za barabarani na vifaa vingine muhimu ili kuhakikisha mpango huu unafanikiwa.

“Dar es Salaam ina uwezo wa kuendesha biashara saa 24. Kariakoo, kama soko linalohudumia mataifa jirani, litachangia kuimarisha uchumi wa mkoa na kuongeza nafasi za ajira,” amesema Chalamila.

Aidha Chalamila amewapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kufikisha taarifa kwa jamii na kusaidia kujenga taifa kupitia ukosoaji wenye lengo la kujenga.

Hata hivyo amewahimiza kuwa waangalifu na taarifa wanazozitoa, hasa zile zinazohusu matukio mbalimbali ikiwemo ya utekaji au kupotea kwa watu.

Ametolea mfano wa tukio la hivi karibuni la mtoto aliyeripotiwa kutekwa, lakini baadaye ilibainika kuwa alipatikana baada ya kuanguka kisimani.

“Hivi karibuni kulikuwa na tukio la mfanyabiashara Daisle Ulomi ambaye aliripotiwa kupotea na madai yakawa yanaonesha kama vile ametekwa, lakini uchunguzi wa polisi ulibaini baadae kwamba alipata ajali ya pikipiki,” amesema.

Amesisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya usalama ili kudumisha amani hasa katika msimu huu wa sikukuu.

Amesema jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi katika kipindi hiki cha sikukuu.

Vilevile ametoa wito kwa wananchi kutembea na vitambulisho ili kurahisisha utambuzi wao katika matukio ya dharura.