Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt Emanuel Nchimbi ameeleza kufurahishwa na kasi ya utekelezaji miradi ya wananchi Mkoani Tabora baada ya kushuhudia baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika Jimbo la Nzega.
Akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali wa mkoa huo wakiwemo wanaCCM mwishoni mwa wiki Wilayani Nzega Mkoani hapa aliwapongeza Wabunge wa Wilaya hiyo na mkoa mzima kwa mshikamano wao mzuri.
Amebainisha kuwa umoja na mshikamano wa qabunge, viongozi, watendaji na wanaCCM ndio msingi wa mafanikio mahali popote pale, hivyo akapongeza kazi nzuri iliyofanyika katika Jimbo hilo na Mkoa mzima.
Balozi Dkt Nchimba ameeleza kuwa ushindi wa asilimia 98 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa huo kwenye uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji ulichochewa kwa kiasi kikubwa na usimamizi mzuri wa ilani ya chama.
‘Ndugu zangu kazi hazidanganyi, mazuri yote yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan yanaonekana na matokeo yake ndiyo haya’, ameeleza.
Aidha amepongeza Kamati za Siasa za Kata na Mabalozi wa nchi nzima kwa kazi yao nzuri na kusimamia vizuri uteuzi wa wagombea hivyo kuwezesha CCM kupata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 99 katika Vijiji, Vitongoji na Mitaa yote.
‘Zaidi ya asilimia 97 ya wagombea waliopitishwa na CCM walikuwa wanakubalika kwa wananchi na wote walishinda kwa kishindo isipokuwa maeneo machache tu ambapo wagombea walikuwa na dosari ndogo ndogo’, amesema.
Alitoa wito kwa Viongozi wote waliopewa dhamana ndani ya chama au serikalini kuendelee kushikamana na kueleza mazuri yote yaliyofanywa na serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi kupitia mikutano yao.
Aidha ameelekeza Viongozi wa Chama na Serikali nchi nzima kuwapa mafunzo maalumu Viongozi wote wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa hivi karibuni ili wajue wajibu wao kwa wananchi na kuwatumikia ipasavyo.
Akiwa Wilayani humo Katibu Mkuu amepokea hundi ya sh mil 50 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo Hussein Bashe kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Ofisi za CCM za kata na kukabidhi vitendea kazi (pikipiki) kwa Viongozi wa kata na matawi.