Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam

TAASISI zote za Serikali zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ambazo  zinahudumia  watu  zaidi ya 100 zimetakiwa kutekeleza bila shuruti  agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  kuwa ifikapo Desemba 31,2024, ziache kutumia nishati chafu zitokanazo  na ukataji wa mkaa . 

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albeth Chalamila ,Mstahiki Meya  wa Halmashauri ya  Manispaa ya Temeke Abdalah Mtinika wakati  kuadhimisha kilele cha Wiki ya Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi na Salama ya Kupikia ijulikayo kama Rafiki Briquettes inayozalishwa  na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Mtinika amesema kuwa kutokana na agizo hilo la Waziri Mkuu matumaini yake ni viongozi wenzake wa Mkoa wa Dar es Salaam watatekeleza agizo hilo bila shuruti hivyo watafanya ukaguzi kwa kila taasisi ili kuona utekelezaji wa agizo hilo.

” Haya tunayoyaona leo ni mapinduzi makubwa katika nishati ambayo yanaenda kuacha alama kubwa kwa vizazi vyetu chini ya mbeba maono Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kuhusu agenda  ya matumizi ya nishati safi na salama ili kuokoa mazingira ambapo  amekuwa ni mpambanaji wa kweli kuhakikisha jamii ya Wàatanzania inaondokana na  matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa inayotokana  na miti ifikapo mwaka 2033″ amesema Mtinika.

Amesema kuwa ubora wa nishati hiyo ya rafiki briquettes  umethibitishwa na shirika la viwango Tanzania (TBS),na kufanyiwa utafiti wakutosha tangu mwaka 2018 na taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Taasisi ya Utafiti na  Maendeleo (TIRDO) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) hivyo niwahimize wananchi kutumia nishati hii ya rafiki Briquettes kutokana haina madhara yeyote kiafya.

Aidha amesema kuwa nishati hiyo ya Rafiki Briquettes inatokana na makaa ya mawe na kuchanganywa na vumbi la sukari guru.

“Makaa ya mawe yanazalishwa kutoka kwenye mgodi wa Kiwira unaomilikiwa na STAMICO uliopo Mkoa wa Songwe ambao una hifadhi ya zaidi ya tani milioni 300 ambazo zitadumu  kwa zaidi ya miaka 100 ijayo hivyo niwatoe hofu wananchi kuwa  kuna siku  moja kutatokea uhaba wa nishati hii ya rafiki briquettes”amesema Mtinika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt Venance Mwasse amesema kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi imekuwa ni tishio dunia mzima hali ambayo imepeleka maifa makubwa kuweka maazimio mbalimbali ikiwemo azimio la kutunza mazingira  lakini pia azimio la kuachana na nishati chafu ambayo inaathili afya za binadamu.

“Kupelekea maadhimio hayo mheshimiwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan alitangazwa kama kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi Afrika na duniani ,sasa sisi kama STAMICO tulitumia ubunifu tukafanya utafiti wa bidhaa tulizonazo  ikiwemo madini tuliyo nayo,rasilimali tulizo nazo ni namna gani na tutumie teknolojia gani sayansi gani ili kubadilisha kwenda kwenye nishati safi  ya kupikia ambayo hii tuliyoizindua”amesema Mwasse.