π Dkt. Biteko ahimiza urafiki Nyabionza na Nyuki FC
π Mshindi wa kwanza aibuka na Milioni 6, wapili Milioni 4
Timu ya Nyabiyonza ya Karagwe mkoani Kagera imeibuka kidedea kwa kuifunga mabao mawili kwa moja timu ya Nyuki FC kutoka Bukombe, mkoani Geita katika mechi ya kirafiki iliyochezwa katika Uwanja wa Bashungwa, Karagwe mkoani Kagera.
Akizungumza Desemba 20, 2024, Karagwe mkoani Kagera mara baada ya mtanange huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri na Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza washiriki wa mechi hiyo na kusema mchezo huo ni sehemu ya kuimarisha umoja, upendo na amani iliyopo.
β Nataka niwahakikishie kuwa watu wa Bukombe watatoka hapa wakiamini ni washindi wa pili, nawapongeza sana makocha wa timu hizi mbili na waamuzi kwa kuamua mpira kwa haki,β amesema Dkt. Biteko.
Pia, amewaasa wananchi wa Karagwe kuishi kwa upendo β Nataka niwasihi watu wa Karagwe kuimarisha umoja wenu kupendana na kuimarisha amani ya wilaya hii,β
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ataendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha Mkoa wa Kagera unapata maendeleo hivyo kuwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kudumisha amani iliyopo ili kuchochea maendeleo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa amefurahishwa na matokeo ya mechi hiyo ya kirafiki kutoka Wilaya ya Bukombe na Karagwe kuisha salama na kuwapongeza wachezaji.
Amesema kuwa mechi hiyo ya kirafiki ilikuwa wazo la Dkt. Biteko mara baada ya timu ya Nyuki kushinda fainali katika mashindano ya ligi ya KNK (Kusema na Kutenda).
βNilipokuja Bukombe kwenye fainali ya KNK Cup ulinielekeza baada ya vijana kushinda fainali ile sasa waje kucheza mechi ya kirafiki Karagwe. Kwa niaba ya wananchi wa Karagwe na Bukombe nakushukuru sana kwa wazo lako ambapo leo limeweza kuleta burudani nzuri kupitia mechi hii,β amesema Mhe. Bashungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amewashukuru Dkt. Biteko na Mhe. Bashungwa kwa kuandaa timu hizo zilizoleta burudani kwa wakazi wa Karagwe.
Mabingwa wa mechi hiyo timu ya Nyabiyonza imenyakua kitita cha kiasi cha shilingi milioni sita, seti moja ya jezi, mpira na kombe wakati mshindi wa pili Nyuki FC akiondoka na kitita cha fedha shilingi milioni nne, seti moja ya jezi na mpira.
Lazaro Peter wa Nyuki FC ameibuka mchezaji bora wa mechi zote mbili huku mlinda mlango bora wa mechi hizo akiwa Rena Mwameja wa Nyabiyonza FC.