Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku, ambapo inatarajia kugawa mitungi 13,020 katika mkoa wa Shinyanga, Mradi huo utagharimu jumla ya shilingi milioni 545.538
REA, iliingia mkataba na mtoa huduma; kampuni ya Lake Gesi, kampuni ambayo, itahudumia wilaya 4 za Mkoa wa Shinyanga kwa kuuza mitungi hiyo ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,950 pamoja na vifaa vyake, katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Hayo yameelezwa na Mhandisi Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini-REA Mhandisi Ramadhani Mganga leo tarehe 19 Disemba 2024 wakati akizungumza na Wakunga, Wauguzi, kina mama waliojifungua watoto njiti na Mama wajawazito katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama na kuwagawia mitungi ya gesi ya Kilo sita kila mmoja ambapo jumla ya mitungi 100 imetolewa yenye thamani ya shilingi Milioni 4.1
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa REA Bi Martha Chassama amesema kuwa kazi ya Serikali ni kuhakikisha nishati safi za kupikia zinawafikia Wananchi wa vijijini kwa ukaribu zaidi na kwa bei nafuu na kuongeza kuwa Serikali inafanya kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.
Chassama amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya gesi hizo walizopewa huku akieleza kuwa wilaya zitakazofikiwa na mradi huo katika mkoa wa Shinyanga ni pamoja na Kishapu, Shinyanga na Halmashauri ya Ushetu na Msalala.
Mbunge wa Vitimaalum Mkoa wa Shinyanga Mhe Santiel Kirumba ameupokea mradi huo ambapo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele na kuipa REA fedha kwa ajili ya kuhakikisha wanawake wanatumia nishati safi na salama ambayo pia itaokoa muda na afya za watumiaji ikiwemo kuokoa mazingira.
“Nishati salama ni mtaji wa afya zetu, ni mkombozi wa uchumi, Inaepusha wanawake na ukatili wa kijinsia, hivyo nampongeza sana Mhe Rais Dkt Samia kupitia taasisi ya REA kwa kumjali mwanamke na watanzania kwa ujumla wake” Amekaririwa Mhe Kirumba.