Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi-PPPC, David Kafulila, amesema Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na afya ya uchumi zaidi ukilinganisha na nchi zote za Afrika Mashariki na nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kauli hiyo ya Kafulila, imekuja kufuatia Ripoti ya Shirika la Fedha Duniani-IMF kuhusu hali ya deni la mataifa 186 Duniani, kuonyesha Tanzania inazidi kuimarika zaidi kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Kafulila, Ripoti hiyo ya Shirika la Fedha Duniani-IMF inaisaidia pia Tanzania kujenga imani kubwa na wawekezaji duniani kuja kuwekeza nchini Tanzania na kuchochea uchumi wake kwa kasi.

Na amesema, inaitangaza Tanzania kwa wafanyabishara na majukwaa makubwa ya uchumi duniani katika kunadi sera zake.

Katika ripoti hiyo inayojulikana kama Economic Outlook ya Oktoba 2024, Tanzania imeorodheshwa na uwiano wa deni kwa uchumi wa Asilimia 47, kiwango kinachothibitisha usimamizi bora wa uchumi ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika na Duniani kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa deni kwa uchumi wa mataifa ya Afrika ni asilimia 67, hii inamaanisha kuwa Tanzania iko mbali chini ya wastani huo, hali inayoashiria uwiano mzuri wa kukopa na matumizi ya fedha za umma.

Inaonyesha kuwa Kenya ina asilimia 70, Rwanda asilimia 71, Uganda asilimia 51, Malawi asilimia 84, Namibia asilimia 67 na Ghana asilimia 84.
Kwa takwimu hizo ni dhahiri Tanzania imedhibiti deni lake vyema zaidi ya mataifa mengi yanayofanana nayo kiuchumi.