Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kampuni ya burudani na masoko ya Starlink Tanzania Limited imekanusha vikali uwapo wa uhusiano wowote na Kampuni ya Starlink Satellite Tanzania Limited inayotoa huduma ya intaneti inayomilikiwa na SpaceX.

Starlink Tanzania Ltd ilisajiliwa Aprili, 2019 na kumilikiwa kikamilifu na Watanzania tofauti na Starlink Satellite Tanzania Ltd inayotoa huduma za satelaiti na kumilikiwa na tajiri namba moja dunia, Elon Musk.

Akizungumza Dar er Salaam leo, Mkurugenzi wa Starlink Tanzania Ltd, Calvin Gibson, amesema kampuni yake imekumbwa na changamoto kubwa ya mkanganyiko wa jina, hali inayosababisha usumbufu kwa wateja na umma kwa ujumla.

“Kampuni yetu haina uhusiano wowote na Starlink Satellite Tanzania Ltd. Matumizi ya jina linalofanana na letu yameathiri hadhi ya brand yetu, na tunachukua hatua stahiki kulinda jina letu dhidi ya kufifishwa,” amasema.

Mkurugenzi wa Starlink Tanzania Limited, Calvin Gibson.

Starlink Tanzania Ltd imesema mkanganyiko huo umechangia maswali mengi kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na kampuni hizo mbili.

“Wateja wanaelekea kuchanganya majukumu na huduma tofauti zinazotolewa na kampuni hizo, jambo linalohatarisha uelewa wa umma na kusababisha madhara ya kiufundi na kibiashara,” amesema.

Pia amesema kampuni hiyo tayari imeanzisha mchakato wa kuchukua hatua za kisheria ili kulinda chapa ya biashara yake na kuhakikisha jina lake halitumiki vibaya.

Hatua hiyo inajiri wakati huduma za Starlink Satellite Tanzania Ltd zimepokelewa kwa shauku kubwa nchini kutokana na ahadi ya kuongeza kasi ya mtandao wa intaneti kupitia teknolojia ya satelaiti.

Starlink Tanzania Ltd imewasihi wateja wake na umma kwa ujumla kutambua tofauti kati ya kampuni hizo mbili, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kutoa huduma bora za burudani na masoko bila mvurugano wa kibiashara.