Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Pwani

Watu wanne akiwemo Meneja wa Kampuni ya GBL Group, Abdul Huot (56) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo ni kopa zenye thamani ya Shilingi Milioni 300 zinazotumika katika miundombinu ya reli ya SGR.

Mbali na Huot ambaye ni raia wa Pakistan washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Kudadad Jalal Bizanjo (63) na Athanas Michael Shija (64). Pia mshtakiwa Dikson Siza (38) ambaye ni mfanyabiadhara amesomewa mashtaka yake peke yake.

Washtakiwa hao ambao wamepewa masharti ya dhamana wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Herieth Mwailolo na Wakili wa Serikali, Recho Mwaipyana.

Wakili Mwaipyana amesema kuwa mshtakiwa Huot, Bizanjo na Athanas Michael kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili ikiwemo kuhujumu ambao walitenda kosa hilo katika tarehe isiyofahamika ndani ya mwezi wa 12 mwaka 2024, ambapo katika maeneo tofauti ya mfumo wa reli ya kisasa ya SGR ndani ya mkoa wa Pwani.

Katika kosa jingine la uharibifu, inadaiwa walilitenda kati ya Disemba 13, 2024 maeneo ya Kisemvule ndani ya Wilaya ya Mkuranga walikutwa na Kilo 5000 za kopa zikiwa na thamani ya Shilingi Milioni 280,000,000/ ambazo zinasemekana zimeibwa.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwailolo alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ambapo Wakili wa Serikali Mwaipyana alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili wa Utetezi Yohana Fungo aliiomba mahakama hiyo kuwapa dhamana washtakiwa hao, ambapo mahakama ilitoa masharti ya washtakiwa hao kuweka bondi ya Shilingi Milioni 100 kwa kila mmoja ama hati ya mali isiyohamishika iliyopo ndani ya mkoa wa Pwani, wasisafiri nje ya mkoa wa Pwani, wawasilishe hati zao za kusafiria, pia wawe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Shilingi Milioni 50 kwa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 3, 2024 kwa ajili ya kutajwa huku washtakiwa wakirudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Katika kesi ya pili, inayomkabili mshtakiwa Siza anadaiwa kutenda makosa mawili ambayo ni uharibifu na kukutwa na mali ya wizi.

Inadaiwa kinyume na sheria, katika tarehe isiyofahamika ndani ya mwezi Disemba 2024, mshtakiwa Siza akiwa katika eneo la Reli ya Kisasa ya Umeme SGR ndani ya mkoa wa Pwani kwa makusudi alifanya uharibifu wa mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika miundombinu ya kusambaza umeme katika wilaya ya Mkuranga.

Katika kosa la pili la kukutwa na mali ya wizi inadaiwa alilitenda Disemba 16, katika maeneo ya Kisemvule ambapo alikutwa na kopa Kilo 200 zikiwa na thamani ya Shilingi Milioni 100 ambazo zimepatikana kwa njia isiyo ya kisheria.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Wakili Mwaipyana amesema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika ambapo Hakimu Mwailolo alisema dhamana ipo wazi kwa washtakiwa.

Mshtakiwa huyo alipewa masharti ya kuweka bondi ya Shilingi Milioni 50 ama hati ya mali isiyohamishika, pia kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani na awe na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa Mkuranga watakaosaini bondi ya Shilingi Milioni 20 kwa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Disemba 30,2024 huku akirudishwa mahabusu kwa kukosa dhamana.