Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Pwani

Watuhumiwa watano, wakiwemo raia wawili wa China, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kibaha na kusomewa mashtaka matano ya uhujumu mali za Shirika la Reli Tanzania (TRC), na kusababisha Serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 200.

Watuhumiwa hao ni Zhang Feng, Wang Yong, Paulo John, Abdul Mohamed Boya, na Pius Kitulya, ambao ni wakazi wa Miwaleni, Mlandizi, mkoani Pwani.

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Joseph Kisaka, aliiambia mahakama kuwa kati ya Novemba na Desemba mwaka huu, watuhumiwa hao walikutwa na nyaya za reli ya kisasa ya SGR zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.

Hata hivyo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, washitakiwa walirudishwa rumande, huku kesi yao ikipangwa kusikilizwa tena Desemba 30, 2024.

Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kibaha, Felista Mweru.