Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

VIJANA nchini wamehimizwa kutumia vizuri vipato wanavyopata kujiwekea akiba ili kumudu maisha yao ya sasa na baadaye.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara Kuu ya Mipango, Fedha Uchumi na Utekelezaji (IMFU) ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Ayoub Sanga wakati akizindua jukwaa la Mapunjo Forum ambalo litakuwa likitoa elimu ya masuala ya fedha, Ujasiriamali na Uongozi.

Amesema kumekuwa na changamoto ya vijana kuweka akiba ya fedha ili iweze kutumia kama mtaji katika kuanzisha biashara au jambo fulani linaloweza kumuingizia kipato.

“Ndio maana leo tunakumbusha kuwa ni wajibu vijana wakapatiwa elimu hizi za utunzaji fedha, ujasiriamali na uwekezaji, nalishukuru jukwaa hili la Mapunjo wameliona jambo hili na wanataka kukikomba kizazi hiki.

“Unapokuwa umetunza fedha na ukasema siwezi kuitumia kwa kufanya kuwa mtaji wa jambo fulani najua ni vigumu na inataka moyo sana hasa kwa hawa vijana, unaweza kumkuta mtu ni daktari, Profesa lakini hajafanikiwa katika biashara kwa sababu jambo la kutunza fedha na kuweka akiba ni gumu kidogo kwake,” amesema Sanga.

Amesema kwa kuwa Jukwaa la Mapunjo litajikita kufanya mijadala mbalimbali ya biashara, uwekezaji na ujasiriamali itasaidia kupanua mawazo ya vijana katika kujitengenezea maisha yao ya baadae.

“Mawazo hasa ya kibuni ndio msingi wa yote kwani yanasaidia katika kuanzisha biashara lakini niwaombe Mapunjo Forum kuangalia namna ambavyo wataweza kulinda mawazo ya watu kwani suala hilo linasumbua sana,” amesema Sanga.

Naye Mwanzilishi na mwenyekiti wa jukwaa hilo, George Mapunjo amesema jukwaa hilo litahusisha na utoaji wa elimu katika masuala ya ujasiriamali, uwekezaji na uongozi.

Amesema kuanzisha jukwaa hilo ni m
ndoto yake ya muda mrefu ambayo alikuwa nao tangu alipokuwa chuo hicho anamshukuru Mungu kwa kuiona inaendelea kuishi.

“Hili jukwaa linakaribia miaka 10 sasa na tulikuwa tukifanya kazi kupitia mitandao ya kijamii, sasa tumeona tuvuke mipaka na tutoke nje tuonane ya watu pamoja na wadau mbalimbali ambao wanahitaji elimu wa kuonana,” amesema Mapunjo.