Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Msafara wa maofisa wa ubalozi wa Uganda hapa nchini ukiongozwa na Balozi Kanali (mstaafu) Fred Mwesigye umesema kuwa umefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) inayoendelea katika maeneo mbalimbali muhimu ya mradi huo , ukiwemo ujenzi wa mkuza wa juu ya bahari wenye urefu wa zaidi ya kilomita mbili unaojengwa katika bahari ya Hindi mkoani Tanga kwa ajili mafuta hayo kupakiwa katika meli kwenda katika masoko ya kimataifa.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, msimamizi wa ujenzi wa eneo hilo Kurt Holtzkausen alisema kuwa tayari wamefikia asilimia 60 ya ujenzi na kazi inaendelea ili kuikamilisha kwa wakati.
Msafara huo pia ulitembelea eneo la Chongoloeani , ambapo Balozi Mwesigye na msafara wake pia ulivutiwa na shughuli mbalimbali, ukiwemo ujenzi wa matenki makubwa manne yenye uwezo wa kuhifadhi mapipa milioni mbili ya mafuta ghafi yatakayotoka Hoima nchini Uganda kwenda Chongoleani.
“Nikiwa kama Balozi, moja ya makujumu yangu ni kutembelea mradi huu ambao tunautekeleza kwa ushirikiano wa wanahisa mbalimbali ikiwemo Serikali ya Tanzania na kutoa ripoti kwa viongozi wangu wakuu wa Uganda;” amesema Balozi Mwesigye.
“Wakati naanza kazi ya Ubalozi hapa nchini mwaka 2022, nilitembelea eneo hili na kukuta kazi za awali zikifanyika ikiwemo usafishaji wa eneo hili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu mbalimbali,”
“Lakini safari hii nimeshangaa kuona maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa mradi huu,” amesema.
Amesema kutokana na kasi ya ujenzi inayoendelea hivi sasa, ana matumaini mradi huu unakwenda kumalizika kwa ufanisi mkubwa na kuleta maendeleo ya kiuchumi baina ya nchi hizi mbili na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.
“Furaha yangu ni kuona mafuta ghafi kutoka Uganda yanasafirishwa hadi katika Pwani ya Chongoleani mkoani Tanga na kwenda nje katika masoko ya kimataifa,” amesema.
Amesema Uganda na Tanzania kwa sasa zinaendelea kunufaika na utekelezaji wa mradi huu katika hatua hii ya ujenzi inayoendelea, ikiwemo wananchi wa nchi hizi mbili kuendelea kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo ajira na wataalam wazawa kubadilisha uzoefu na wataalam wa kigeni kutoka nchi mbalimbali katika maeneo tofauti tofauti.
Mhandisi Musa Msafiri wa eneo la Chongoleani alisema kuwa kasi ya ujenzi inaendelea, ambapo tayari ujenzi wa matenki hayo umefikia asilimia 69.8.
“Mategemeo yetu ni kumaliza ujenzi wa mradi huu kama inavyokusudiwa, ambapo kwa sasa kuna baadhi ya maeneo ya ujenzi tayari yamefikia hatua nzuri ya utekelezaji na baadhi ya maeneo kazi bado inaendelea,” amesema.
Akiongea katika ziara hiyo iliyojumuisha maofisa wengine mbalimbali waandamizi wa ubalozi huo hapa nchini akiwemo Naibu Balozi Elizabeth Allimadi, Mhandisi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mafuta nchini Uganda (PAU) Injinia Deo Bukenya amesema maendeleo ya mradi huo yaliyofikiwa hivi sasa ni ya kujivunia ili kukamilisha ndoto ya mradi huo.
“Tumefurahishwa na namna kazi inavyoendelea kwa kasi kwa ushirikiano mkubwa kati ya wafanyakazi wa kigeni na wazawa,”
“Kwa upande wa Uganda, mradi huu pia unaendelea vizuri kama ilivyo hapa Tanzania ambapo utekelezaji wake kwa kiasi kikubwa unafanyika ukihusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali muhimu ,” amesema.
Miongoni mwa miundombinu muhimu ya mradi huo hapa nchini ni kiwanda cha kuweka mfumo wa joto katika mabomba yote yatakayofukiwa chini ya ardhi kwa ajili ya kusafirisha mafuta ghafi kilichopo Sojo, Wilayani Nzega mkoani Tabora.
Mbali na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu, Injinia Bukenya pia ameoneshwa kufurahishwa na namna mradi unavyotunza mazingira, kushirikiana na jamii zinazoishi pembezoni mwa mradi na kuzingatia usalama wa wafanyakazi wake.
Msafara huo pia ulitembelea eneo la Mto Sigi, ambapo mkandarasi anaweka miundombinu ya kupitisha bomba la kusafirisha mafuta ghafi chini ya mto huo bila kuathiri mazingira yake.
Meneja wa mradi wa eneo hilo Sinan Elaslan amesema kazi inayofanyika ni kuhakikisha bomba hilo linapita chini ya mto katika umbali mrefu ili lisiathiri maisha ya viumbe wanaoishi ndani ya mto huo wakiwemo samaki.
Mradi wa EACOP ambao unapita katika mikoa nane hapa nchini, una urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi rasi ya Chongoleani mkoani Tanga.
Kati ya kilomita hizo, kilomita 1,147 za mradi huo zipo nchini Tanzania na zilizobaki zipo nchini Uganda.
Wanahisa wa mradi huu ni TotalEnergies yenye asilimia 62, wakati Mashirika ya Maendeleo ya mafuta (TPDC- Tanzania na (UPDC kwa upande wa Uganda ) yana miliki asilimia 15 kila moja na shirika la mafuta la China (CNOOC) linamiliki asilimia nane tu katika mradi huu