Israel imethibitisha kufanya mashambulizi dhidi ya meli za kivita za Syria, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuondosha mali za kijeshi nchini humo baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad.

Katika taarifa yake jeshi la ulinzi la Israel (IDF) limesema meli zake zilishambulia bandari za Al-Bayda na Latakia Jumatatu usiku, ambapo meli 15 zilitia nanga.

BBC imethibitisha video zinazoonyesha milipuko katika bandari ya Latakia, huku picha nyingine za video zikionyesha uharibifu mkubwa kwa meli na sehemu za bandari.

IDF pia imesema ndege zake za kivita zimefanya mashambulizi zaidi ya 350 ya anga katika maeneo mbalimbali nchini Syria, wakati yakihamishia vikosi vya ardhini katika eneo la mpakani kati ya Syria na milima ya Golan inayokaliwa na Israel.

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza (SOHR) lilisema kuwa limerekodi zaidi ya mashambulizi 310 yaliyofanywa na kundi la IDF tangu serikali ya Syria ilipopinduliwa na waasi siku ya Jumapili.

Katika taarifa, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alisema IDF inalenga “kuharibu uwezo wa kimkakati ambao unatishia taifa la Israeli”.