Benki ya Dunia yapunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Kenya 2024 hadi asilimia 4.7 kutokana na changamoto za kifedha

Benki ya Dunia imepunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Kenya kwa mwaka huu hadi asilimia 4.7 siku ya Jumanne, kutoka asilimia 5.0 ya awali, ikitaja athari za mafuriko, maandamano ya kuipinga serikali na juhudi za kuimarisha fedha.

Taifa hilo la Afrika Mashariki limefanikiwa kuimarisha kiwango chake cha ubadilishaji wa fedha za kigeni, kuongeza akiba ya fedha taslimu katika benki kuu na kupunguza mfumuko wa bei mwaka huu, lakini bado inakabiliwa na hatari kubwa ya kukumbwa na madeni, Benki ya Dunia imesema katika ripoti mpya.

“Udhaifu wa madeni ikiwa ni pamoja na gharama za juu za kuhudumia madeni, kukusanya bili zinazosubiriwa, na ukosefu wa malengo ya mapato bado ni changamoto kubwa,” benki hiyo ilisema katika ripoti kuhusu uchumi wa Kenya , ambayo kwa kawaida huchapishwa mara mbili kwa mwaka.

Ingawa makadirio ya ukuaji wa mwaka huu ni ya chini kuliko kiwango cha mwaka jana cha 5.6%, bado ukuaji huo ni wa juu kuliko wastani wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wa 3.0%, benki hiyo ilisema.

Ukuaji wa Kenya hatahivyo, utafikia asilimia 5.1 katika kipindi cha kati, ilisema, ikiwa serikali itafanikiwa kukabiliana na changamoto za kifedha.