Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

IMEELEZWA kuwa wazazi wana jukumu la kuwaendeleza watoto wao kwa kuwapatia elimu bora na kuwafundisha stadi za maisha.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Mdau wa Elimu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Fahari Africa Group Limited, Pius Kishiki wakati wa maadhimisho ya miaka nane ya Coach Ally Educational Supporters sambamba na mahafali ya kidato cha Nne yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Afya cha Msongola, jijini Dar es Salaam.

Amesema elimu ndio ufunguo wa maisha na njia ya kumsaidia mtoto kuondokana na ujinga pamoja na kuwa na maisha bora.

“Nichukue fursa hii kutoa wito kwa wazazi watengenezee Mazingira mazuri ya elimu watoto wao ili wasije kusumbua baadae.

“Huwezi kuwa daktari, Mbunge, Injinia au kiongozi mkubwa kama huna elimu. Na kidato cha nne ndo njia au ufunguo wa kufikia mafanikio ya aina mbalimbali,” amesema.

Aidha ametoa wito kwa wanafunzi ambao watashindwa kujiunga na kidato cha tano waweze kujiendeleza kupitia vyuo vya ufundi huku akibainisha kuwa ili kufanikiwa katika maisha lazima kuwa na taaluma rasmi, fani za aina mbalimbali pamoja na kipaji.

Awali akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wengine, Happy Ezdon amesema Coach Ally Educational imeweza kuwasaidia wanafunzi wengi hasa wanaoishi ukanda wa Chanika na maeneo ya jirani kuweza kufaulu kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu Chuo cha Msongola, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Msongola, Dkt. Alex Mwita anatoa wito kwa wanafunzi watakaofeli kidato cha nne, waweze kujiunga na chuo hicho katika fani ya utabibu pamoja na ufundi.

“Kwanza Mazingira yake ni rafiki, kina nyenzo nyingi za kufundishia, ni Chuo chenye walimu mahiri na ada yake ni nafuu. Hiki ni Chuo kimoja wapo chenye matokeo mazuri, baadhi ya wanafunzi waliohitimu hapa wanasoma udaktariā€¦tangu tuanze wameshahitimu wanafunzi 120 wa ngazi wa Diploma ya utabibu na katika hao wanafunzi 110 wametoka na ufaulu vizuri,” amesema.

Naye Chuo Mkurugenzi Chuo cha Ufundi Msongola, Iman Athmani, amesema Chuo hicho kimeanzishwa takribani miaka saba na kwa kuangalia mahitaji ya watu wengi muhimu wakaamua kuanzia kozi za ufundi stadi.

“Makusudi haya yalikuja baada ya kuona asilimia kubwa ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne wanapotea mtaani. Tukaona ili kusaidia wanafunzi hawa ni muhimu kuanzisha kozi za ufundi stadiā€¦.hapa chuoni kwetu tuna kozi tano za ufundi stadi ambazo ni kozi ya ufundi umeme wa majumbani, sekretari, Tehama(ICT), Hotel Management na Utalii na kozi ya Ualimu wa Chekechea na Malezi ya watoto,” amesema.