Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kupokea meli kubwa za mizigo katika bandari yake ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mafanikio baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika katika bandari hiyo uliopeleka maboresho mbalimbali ya utendaji na utoaji huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw Plasduce Mbossa kwenye hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo inayoitwa EverGreen Line Group ikitokea nchini China yenye uwezo wa kusafirisha zaidi ya makontena elfu nne, Meneja wa Zimamoto na Usalama wa mamlaka hiyo TPA, Bw. Mussa Biboze alisema kuwa uwekezaji na uboreshwaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo umekuwa ukiwavutia wawekezaji pamoja na mawakala mbalimbali wa makampuni za meli kuleta meli zao kupitia Bandari hiyo.
“Uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia TPA katika Bandari ya Dar es Salaam umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji na hivyo kuvutia kampuni kama EverGreen Line Group kuleta meli yake kwenye bandari yetu,” alisema Bw. Biboze.
Alisema miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja uwepo wa kamera za Ulinzi na Usalama za kutosha katika eneo lote la Bandari pamoja na kuongezeka kwa krane ambazo zinasaidia kushusha na kupakia makontena ndani ya muda mfupi sana, hivyo kufanya meli isitumie muda mrefu kukaa hapo bandarini tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Alisema mara ya mwisho kampuni hiyo kuitumia bandari ya Dar es Salaam ilikuwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini wamerudi tena baada ya maboresh makubwa yaliyofanywa na wawekezaji wakiwemo DP World na Adan International Ports Holding .
‘’Napenda kukiri kuwa makampuni haya yanayosimamia gati hizi yameongeza tija kwa Serikali pamoja na kuongeza mapato, lakini pia kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaotumia bandari ya Dar es salaam’’ alisema Bw. Biboze.
Bw. Biboze alisema ujio wa meli kama hiyo utaongeza mapato kwa TPA na TRA, huku ukitoa fursa kwa madereva wengi zaidi ambao watahitajika kwa ajili ya kusafirisha mizigo iliyopo ndani ya makontena hayo.
Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania, Bw. Mohamed Lotfy alisema hapo awali walikuwa wanaleta mizigo kupitia meli ndogo, lakini hivi sasa wameamua kuja na meli kubwa na hiyo yote ni kutokana na maboresho makubwa katika utoaji huduma yaliyofanyika katika bandari hiyo.
‘’Utafiti tulioufanya umetupa nguvu ya kuleta meli yetu kubwa ambayo ina uwezo wa kubeba makontena elfu nne,”
“Hivyo, tutakuwa na safari moja kila mwezi na baadae tutakuwa na safari mbili kwa mwezi ili tuweze kuleta mizigo zaidi, alisema, Bw. Lotfy.
Naye Meneja Kitengo cha Biashara na Mahusiano wa Tanzania East Africa Gateway Terminal Ltd. Bw. Donald Talawa alisema ni mafanikio makubwa kupata meli kama hiyo yenye uwezo wa kuchukua makontena mengi zaidi kwa wakati mmoja.
‘’Sisi tuko tayari kuipokea na kuihudumia meli hii ambayo ni mpya na ya kisasa ambayo imekuja moja kwa moja kutoka nchini China,”
“Napenda nikiri kwamba maboresho yaliyofanywa hapa Bandarini yanaruhusu aina ya meli kama hizi kufika kwa sababu ya kuongezwa kwa kina cha bandari’’ alieleza Bw. Talawa.
Hafla hiyo ya upokeaji wa meli hiyo pia ilihudhuriwa na Meneja Udhibiti wa Huduma za Meli kutoka katika Shirika la uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bi. Fatma Masenene .
Bi.Fatma alisema ujio wa meli hiyo ni neema kwa Serikali kwa sababu inapata mapato, wamiliki wa bandari kavu, na wafanyabiashara wa bidhaa ndogo ndogo kama vile wa vyakula na maji na hata watu wa usafi watafaidika pia.