Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa wanne kwa mauaji ya mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Simbayao.
Watuhumiwa hao ni makuli na wakazi wa Tegeta kwa Ndevu, Dar es Salaam, Deogratius Massawe (40) na Bakari Bakari. Pia wapo mpigadebe, Omary Issa Mkazi wa Tegeta Dawasco na dereva wa pikipiki maarufu ‘Bodaboda’, Rashid Mtonga (29).
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema watuhumiwa wote wanne na wengine wanahojiwa kwa kina.
Alisema mbali na mauaji hayo, watuhumiwa walimjeruhi mtumishi wa TRA, Adriano Fredrick na kuharibu gari lenye namba za usajili STL 9923 aina ya Toyota LandCruiser Hardtop yenye rangi nyeupe, mali ya TRA.
“Tukio hili lilitokea Desemba 5, mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku maeneo ya Tegeta kwa Ndevu Kinondoni, maofisa wa TRA walikamata gari aina ya BMW X6 yenye namba za usajili T 229 DHZ ambayo waligundua kwamba iliingizwa nchini kinyemela bila kulipiwa kodi za serikali kwa mujibu wa sheria,’’ alisema Muliro.
Alieleza kuwa maofisa hao walikuwa wakitekeleza majukumu yao kisheria na walifuata taratibu za kisheria dhidi ya mtuhumiwa.
Hata hivyo, lilijitokeza kundi la watu ambao waliwashambulia kwa mawe na kuharibu gari na kusababisha kifo cha mtumishi huyo wa serikali.
“Jeshi la polisi linawaonya na halitavumilia watu ambao wanataka kujenga tabia ya kushambulia watumishi wa serikali wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kisheria licha ya kufuata taratibu za kiutendaji,’’ alisema.
Pia, alisema tabia hiyo inataka kujengeka kwa sababu mbalimbali ambazo hazikubaliki na kwamba hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria na za haraka dhidi ya wahusika kwa kuwakamata, kuhoji na kuwapeleka kwenye mamlaka nyingine za kutenda haki.
Kadhalika, alisema hawatavumilia fikra zinazoashiria kuwa mauaji hayo yalikuwa halali kwa sababu ya matukio ya mauaji na utekaji.
Alisema haikubaliki suala la kujichukulia sheria mkononi kwamba lazima wahusika watawaingiza kwenye msukosuko wa kisheria kwa kutafsiri matendo ya hovyo watakayoyatenda.
“Tusitembee na move (mtazamo) kwamba polisi wakitaka kukamata wahalifu wajiulize wataaminije kama ni polisi, hatuwezi kwenda kwa mtazamo huu, wahuni wanaojifanya polisi na watumishi wa serikali watashughulikiwa kisheria kama ilivyokuwa siku za nyuma na wakapotea. Hatuwezi kuhalalisha kushambuliwa kwa maofisa wa serikali kutokana na mtazamo unaojengeka,’’ alisisitiza.
Alisema masuala mengine ya uchunguzi yanaendelea dhidi ya tuhuma hizo na kwamba kwa ushahidi wanaokusanya watafikisha kwa mamlaka zinazotengeneza mashitaka kwa hatua zaidi.
Kwa mujibu wa TRA, kifo cha Simbayao kimetokea Desemba 6, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikolazwa kwa baada ya tukio la shambulio akiwa katika majukumu yake ya kazi kwa maslahi ya taifa.
Hata hivyo, waliomba wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.