Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Tume ya Ushindani (FCC) inachagiza wawekezaji kujitokeza na kuchangamkia fursa za kuwekeza katika sekta ya utalii na uchumi wa bluu wilayani Mafia.

Tume hiyo imesisitiza kuwa ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuingia sokoni bila hofu ya ushindani wa kibiashara, ili waweze kujitengenezea nafasi, kukuza mapato, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza wakati wa Mafia Festival, Mkurugenzi wa Tafiti, Miungano ya Makampuni, na Uraghbishi wa FCC, Zaytun Majid Kikula, alisema dhamira kuu ya tume hiyo ni kukuza ushindani wa haki na kumlinda mtumiaji kwa kuzuia vitendo visivyo vya kiushindani.

“Wawekezaji wanapaswa kujenga mahoteli ya kisasa bila ubinafsi, ili kila mmoja mwenye uwezo apate nafasi ya kuleta ushindani wa kweli,” alisema Kikula.

Aidha, alitoa tahadhari kwa wawekezaji dhidi ya vitendo vya kiutendaji visivyokubalika, kama kupanga bei kwa pamoja au kutumia vibaya nguvu ya soko.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Hifadhi ya Bahari wilayani Mafia, Daniel Mallya, alisema usafi wa fukwe za bahari ni kipaumbele katika kuvutia watalii na wawekezaji. Alibainisha kuwa hifadhi hiyo imeanzisha utaratibu wa kufanya usafi kila mwezi pamoja na kutoa elimu kwa jamii.

Hata hivyo, Mallya alieleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni uchafuzi wa mazingira unaotokana na kilimo cha mwani kinachotumia chupa za plastiki, ambazo huishia kuenea pembezoni mwa bahari.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, alisema Mafia ni eneo salama na lenye mvuto kwa wawekezaji.

“Wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza katika fukwe zetu ili kuvutia watalii na kuchochea maendeleo ya wilaya,” alisema Mangosongo.

Aidha, alibainisha kuwa tamasha la Mafia, ambalo sasa linafanyika kwa mara ya pili, limeanza kuonyesha mafanikio makubwa, hususan katika ongezeko la watalii na wawekezaji.