MKOA wa Arusha utaadhimisha miaka 63 ya Uhuru kwa kufanya kongamano kubwa la maombi kwa ajili ya kuombea mkoa huo dhidi ya changamoto zinazokumba jamii ya mkoa wa kaskazini mwa Tanzania

Akizungumzia madhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ametangaza kuwa Desemba 9,2024 wakati Tanzania itakapoadhimisha miaka 63 ya Uhuru, mkoa huo utafanyika kongamano kubwa la maombi.

Rc Makonda ametoa kauli hiyo alipokutana na kuzungumza na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Arusha na kusema katika maadhimisho hayo kutafanyika pia matembezi maalum kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha yakijumuisha viongozi hao wa dini na wananchi wa mkoa wa Arusha.
“Tutatembea kwa pamoja maeneo mbalimbali mkoani Arusha tukiwa na bendera, tukitamka maneno ya baraka na maombezi kwa Mkoa wetu wa Arusha tukiombea amani, baraka, biashara zetu pamoja na kizazi tukitakacho mkoani Arusha,” amesema Makonda.

Kauli ya Rc Makonda inakuja wakati huu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kufuta sherehe za kitaifa za maadhimisho ya uhuru kwa mwaka 2024 na kuelekeza yafanyike katika ngazi ya mikoa huku pia akitaka fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili ya sherehe hizo zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya viongozi wa dini akiwemo Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Shaban Juma amesisitiza maombezi hayo ni kheri katika mkoa na nchi kwa ujumla huku mwenyekiti wa wajasiamali Mkoa wa Arusha, Husna Almasy amesisitiza wajasirimali kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwaajili ya kufanya maombi kwani wajasiamali ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi kimkoa, kitaifa na hata kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).