Na Lookman Miraji

Wahitimu wa chuo cha bahari cha Dar es salaam (DMI) wameaswa juu ya kuweka mbele suala la uzalendo katika fani hiyo kwa manufaa ya taifa.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa uchukuzi , David Kihenzile katika hafla ya mahafali ya 20 ya chuo hicho.

Naibu Waziri Kihenzile ametoa rai hiyo kwa wahitimu, bodi ya chuo pamoja na menejimenti ya chuo hicho kufanya bidii kuhakikisha wahitimu wanaendelea kuwa na moyo wa uzalendo katika fani hiyo kwa manufaa makubwa ya taifa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kwa kutoa ombi kwa uongozi wa chuo hicho kuhakikisha unashirikiana kwa karibu na kampuni mbalimbali za usafirishaji na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji katika kuhakikisha wanatakeleza malengo ya chuo hicho.

Kwa upande wake nae mkuu wa chuo hicho Bi: Tumaini Gurumo amewataka wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata chuoni hapo kuleta maendeleo chanya katika sekta ya bahari nchini.

Mahafali hayo yanakuwa mahahafali ya 20 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho ambapo jumla ya wahitimu 1529 wamehitimu masomo yao katika ngazi tofauti tofauti.