Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka madereva Nchini wameaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuondokana na ajali zisizo za lazima.

Hayo yamesemwa na mkuu wa operesheni wa Kikosi cha usalama barabarani Tanzania, Kamishina Msaidizi wa Polisi ,Nasoro Sisiwaya akiwa eneo la Chamakweza Chalinze Mkoani Pwani .

Amewataka madereva kote nchini kutambua swala la kutii Sheria za barabarani siyo hiyari bali ni la lazima.

Sisiwaya amekemea vitendo vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani vinavyofanywa na baadhi ya madereva kwa makusudi ambavyo baadhi ya vitendo hivyo vimekuwa ni chanzo chanzo cha ajali zinazo sababisha vifo na majeruhi.

Katika operesheni hiyo madereva 21 wa magari binafsi, magari yasafirishayo abiria kwenda mikoa mbalimbali na yale yafanyayo safari zake ndani ya Mkoa walikamatwa na kuonywa baada ya kubainika kuvunja sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani ,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Edson Mwakihaba amewasihi madereva wa vyombo vya moto kubeba abiria kulingana na kadi ya gari ilivyoelekeza.