Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Baraza la michezo la taifa imetoa baraka zake kwa timu ya taifa ya mchezo wa kuogelea inayotarajia kwenda kushiriki mashindano ya dunia yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni huko Budapest nchini Hungary.
Akizungumza wakati wa ukabidhiwaji wa bendera kwa timu hiyo ya taifa ya kuogelea, Afisa michezo kutoka Baraza la michezo la taifa (BMT), Bi: Ingrid Kimario amesema kuwa wao kama serikali wanatambua jitihada kubwa zinazofanywa na viongozi wa mchezo huo wa kuogelea nchini pamoja na viwango vizuri vinavyooneshwa na waogeleaji wa kitanzania katika ushiriki wao kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki kimataifa .Hivyo kwa kuzingatia hilo serikali imetoa fedha takribani shillingi za kitanzania Millioni 20 kuiwezesha timu hiyo kuelekea katika mashindano ya dunia yatakayoanza hivi karibuni.
Aidha Afisa Ingrid Kimario ameongeza kuwa serikali ina matumaini makubwa kwa timu hiyo juu ya uwakilishi wa taifa katika mashindano hayo makubwa duniani.
Kwa upande mwingine mwenyekiti wa chama cha kuogelea (TSA) , David Mwasyoge ametoa shukrani kwa serikali kwa kutambua mchango wa mchezo wa kuogelea katika kuliwakilisha taifa ambapo pia ameongeza kuwa mashindano hayo ni sehemu nzuri kwao kama viongozi wa chama na wachezaji kuendelea kujiweka sawa zaidi kuelekea katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2028.
Wachezaji nao wa timu hiyo ya taifa wakiongozwa na nahodha wao Collins Saliboko pamoja nae muogeleaji Lina Goyayi wamejinasibu kuwa wamejiandaa vizuri huku wakiamini kuwa wanakwenda kuvunja rekodi zao za awali ili kuonesha kuwa mchezo huo wa kuogelea unazidi kupiga hatua siku hadi siku.
Timu hiyo ya taifa imesafiri na waogeleaji wa wanne pamoja na viongozi wa chama cha kuogelea pamoja na muwakilishi wa serikali ambaye ni kaimu katibu mkuu mtendaji wa baraza la michezo la taifa atakayeambatana na timu hiyo katika mashindano hayo.
Wachezaji wanaounda timu hiyo ya taifa ni
Collins Saliboko, Aliyana Kachra, Lina Goyayi na Michael Joseph.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza rasmi mnamo Disemba 10 na kumalizika Disemba 15 huko nchini Hungary.