Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Taasisi ya Wiloses Foundation imekabidhi mashine mbili zenye thamani ya sh. Milioni 10.5 katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea (HOMSO) ambazo zitasaidia watoto wachanga na wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) kusaidia kupumua na kurekebisha joto la mwili.
Wiloses Foundation ni shirika lisilo la kiserikali ambalo linajishugulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo ya kusaidia akina mama, watoto na maswala mengine ya kisheria ambalo makao mkuu yake yapo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mashine hizo Hospitalini hapo,Mkurugenzi wa Taasisi hiyo,Dkt.Geofrey Mdede amesema kuwa kutokana na changamoto ya kukosekana kwa mashine za kusaidia watoto kupumua na kurekebisha joto la mwili yeye na mke wake waliamua kuzinunua ili kuondoa tatizo hilo.
“”Mwaka 2023 tulikaa tukafikiri kwamba ni jambo gani tutalifanya,mimi na mke wangu na sisi wote ni maktari na tumefanya kazi katika hospitali hii, Mimi binafsi nimeanza kupanda vyeo nikitokea hapa kwa hiyo hospitali ambayo mimi nahifahamu na nikaona lazima nianze nyumbani ambapo mimi niliona pana changamoto basi nisaidie taasisi ya serikali kwaajiri ya kuweza kusaidia watoto wachanga na wanaozaliwa kabla ya wakati “alisema Dkt.Mdede.
Kwa upande wake kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma Dkt.Revocatus Makaranga ameishukuru Taasisi ya Wiloses Foundation kwa msaada wa vifaa tiba ambavyo ni mashine mbili ambazo zitasaidia kuboresha huduma za kitengo cha watoto wachanga.
“Kitengo chetu kinalaza na kutoa huduma takribani watoto 85 kwa mwezi kitengo ambacho kinatoa huduma mbalimbali kwa watoto wachanga wakiwemo waliozaliwa kabla ya kufikisha miezi 9 (Njiti) ,watoto waliopata homa ya Manjano baada ya kuzaliwa pamoja na watoto waliozaliwa baada ya kufikisha miezi 9 na wakapata changamoto nyingine mbalimbali za kiafya “alisema Dkt. Makaranga.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika afla hiyo fupi ya kukabidhi mashine hizo katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bi.Mary Makondo ameipongeza Taasisi ya Wiloles Foundation kwa kuwa na maono ya kununua vifaa tiba kwaajiri ya kusaidia watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto mbalimbali.
Alisema kuwa changamoto mbalimbali wanazopata watoto wachanga zinauhusiano wa moja kwa moja na huduma alizopewa mama akiwa mjamzito, wakati wa kujifungua na punde baada ya kujifungua hivyo pamoja na mahitaji mengine ikiwemo uwepo wa vifaa tiba ambayo nguzo muhimu.
“Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria wa mwaka 2022 nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, hata hivyo vifo kwa upande wa watoto wachanga katika Mkoa wa Ruvuma mwaka 2015 vilikuwa 7 kati ya watoto 1000 na mwaka 2022 vifo vilikuwa 5 kati ya watoto wachanga 1000.”alisema katibu tawala huyo Makondo.
Alisema kuwa sababu kubwa ya vifo vya watoto wachanga kwa Mkoa wa Ruvuma ni pamoja na tatizo la kupumua wakati wa kuzaliwa ,Njiti,uambukizo, malaria na Pneumonia.
Hata hivyo ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza na kuendelea kuchangia vifaa tiba kwani uhitaji bado ni mkubwa na kwamba ni jambo jema sana katika jamii inayotuzunguka.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Louis Chomboko alisema kuwa changamoto zipo nyingi kwa watoto wachanga ambapo anaweza akazaliwa mtoto Njiti akapata matatizo ya kupumua,akapata maambukizi,akapata pia vitu vingine ambavyo vitafanya maisha yake katika hali ile ya uchanga kuwa kwenye hatari.
Alisema kuwa Kila pumzi inathamani lakini Kila mtoto anathamani hivyo kama Mkoa wanaendelea kuchukuwa hatua pamoja na juhudi mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hizo ambazo watoto wachanga wanazipata pindi wanapozaliwa.
” Mkoa katika hospital zake 18 asilimia 62 ya hospital hizo zinatoa huduma za kusaidia watoto wachanga wanaopata changamoto mbalimbali baada ya kuzaliwa ikiwemo kupumua na kwamba huduma hizo ni endelevu”
Mwakilishi upande wa wananchi aliyefika kwenye afla hiyo Mhandisi Koyoya Fuko ameishukuru Taasisis hiyo ya Wiloses Foundation kwa kuona umuhimu wa kusaidia vifaa tiba hivyo ambayo vitasaidia kuokoa maisha ya watoto wachanga pindi wanapozaliwa na matatizo mbalimbali lakini amewaomba watu binafsi wenye uwezo,mashirika mengine binafsi kujitokeza kusaidia huduma hizo za vifaa tiba kwa watoto wachanga.