Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali inatarajia kuzindua rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Desemba 11, 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.

Hayo yalisemwa Ijumaa, Desemba 6, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Prof. Mkumbo alisema mgeni rasmi katika tukio hili anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Uzinduzi huo unakuja baada ya zoezi la ukusaywaji wa maoni kutoka kwa wananchi na wadau wa maendeleo 1.17 milioni kati ya Desemba mwaka jana na Oktoba mwaka huu.

Wananchi na wadau hao walitoa maoni kwa njia za tafiti katika ngazi ya kaya, ujumbe kwa njia ya simu (USSD), tovuti, makongamano, mahojiano mahsusi na ya kina na viongozi mbalimbali waliopo madarakani na waliostaafu, mikutano na semina na nyaraka zilizokusanywa.

“Uzinduzi wa Rasimu ya Dira 2050 utaenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wadau. Awamu hii itahusu maoni ya uhakiki wa Rasimu ya Dira 2050 (validation),” alisema Prof. Mkumbo.

Mhe. Waziri alisema zoezi la kukusanya maoni ya uhakiki litahitimishwa Januari 18, 2025 kwa Mhe. Waziri Mkuu kupokea rasimu ya pili ya Dira 2050 iliyoboreshwa kutokana na maoni ya wadau katika hatua ya uhakiki.

Aliongeza kuwa kati ya Januari na Machi 2025, Rasimu ya Dira 2050 itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika vyombo vya serikali (Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango na Baraza la Mawaziri).

Baada ya hapo, Mhe. Waziri aliongeza, kati ya Aprili na Mei 2025, Rasimu ya Dira 2050 itapokelewa, kujadiliwa na kuidhinishiwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Mei/Juni 2025.

“Maandalizi ya Dira 2050 yanaenda sambamba na maandalizi ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo (Long-Term Perspective Plan – LTPP) utakaotafsiri maono na matamanio yaliyopo katika Dira 2050,” alisema Prof. Mkumbo.

Alihitimisha kwa kusema: ”Dira hii ni ya Watanzania wote na naomba kuwasihi Watanzania wote washiriki kikamilifu katika hatua zote hadi siku rasmi ya Uzinduzi.”

Akiongea kwa niaba ya vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Bw. Deodatus Balile alisema anapenda kuona Tanzania itakayo tengeneza mazingira ya Serikali kuwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari.

“Lazima tuwe na utamaduni wa Serikali kuwafikishia wananchi taarifa, na Serikali kupata taarifa kutoka kwa wananchi,” alisema Bw. Balile.

Sanjari na hilo, alieleza shauku yake ya kuona Tanzania inayotoa kipaumbele kwa sekta ya viwanda na elimu bora.

“Ili tuweze kulipeleka mbele Taifa letu la Tanzania, lazima Dira ya Taifa iwe chombo kinachounganisha Taifa kwa muktadha kuwa mabadiliko yoyote ya viongozi yasije yakapelekea mabadiliko ya vipaumbele vilivyopo kwenye Dira,” alihitimisha Bw. Balile.