Rais Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini ambaye alitangaza sheria ya kijeshi ametakiwa kuondoka kwenye chama chake cha People’s Power Party.

Kiongozi wa chama hicho Han Dong-hoon aliwaambia waandishi wa habari “amemtaka rais huyo kujiuzulu” kutoka kwa chama.

Hata hivyo chama hicho kimedokeza kuwa hakitaunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani iliyoletwa na upinzani.

Yoon amekubali kujiuzulu kwa waziri wa ulinzi Kim Yong-hyun, ambaye inasemekana ndiye aliyependekeza sheria ya kijeshi kwa rais.Kim aliomba radhi kwa baraza la mawaziri hapo jana na kujiuzulu.

Maandamano zaidi na mikutano ya hadhara inafanyika kote nchini humo hii leo huku rais – ambaye sasa anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye – akitarajiwa kuomba msamaha.

Bunge linatazamiwa kupiga kura ya kumuondoa Yoon madarakani.