Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Wathibiti ubora wa shule za sekondari na vyuo nchini, wamehimizwa kukaa mguu sawa kuhakikisha elimu ya amali inatekelezwa ipasavyo kutokana na mafunzo wezeshi yaliyotolewa ili jamii na serikali ziweze kufikia malengo yao.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne Jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Mahera amesema, lengo la mafunzo ni kuwawezesha wathibiti hao kufanya tathmini ya elimu ya amali kwa ufanisi ili kukidhi mahitaji ya mabadiliko na mageuzi yanayofanywa na serikali katika mtaala wa elimu ya sekondari katika eneo la amali.
Aidha Dkt. Mahera amefafanua kuwa mageuzi hayo kielimu yanalenga kutoa elimu bora kwa kuandaa wahitimu wenye ujuzi, maarifa, stadi, ubunifu na mwelekeo chanya na wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa na kukidhi mahitaji ya soko la ajira nchini, Kikanda na Kimataifa.
“Nawahimiza katumieni maarifa, ujuzi na ubunifu wote mlioupata katika mafunzo haya kwa kutekeleza kwa vitendo katika kuwawezesha wadau wote wa elimu waliopo kwenye maeneo yanayowazunguka ili amali ilete tija kwa taifa na jamii kwa ujumla” amefafanua na kuongeza,
“Ni imani yangu kuwa mtakwenda kuyatekeleza kwa ufanisi yote mliyowezeshwa na wataalam hawa, mkaambukize ujuzi mlioupata kwa wathibiti ubora wa shule wenzenu, maafisa elimu wa wilaya na kata, watendaji wa serikali, vyama vya siasa, walimu, wanafunzi na jamii yote” ameeleza Dkt Mahera.
Kwa upande wake Kamishna wa Elimu Nchini Dkt. Lyabene Mtahaba amewaasa wathibiti ubora wa shule kujenga mazingira ya urafiki kwa watumishi ili kuwaondolea uwoga na mashaka katika utendaji kazi.
“Msiende kutengeneza roboti, maana ukifanya kazi kwa kukosoa, kukemea na kuelekeza, unamuondolea mtumishi kujiamini, hamasa na utayari wa kufanya kazi, shirikianeni na kuelekezana, mambo yataenda vizuri na mafanikio ya mafunzo haya yataonekana” amefafanua Dkt Mtahaba.
Vile vile Mwenyekiti wa Mafunzo Levina Lemomo amesema kutokana na mafunzo hayo muhimu wataenda kufanya tathmini kwa nadharia na vitendo katika utekelezaji wa amali shule za sekondari na vyuo.
“Tutatoa maoni yenye tija na kuboresha sambamba na kupitia asasi tulizonazo, na tunatamani shule za amali ziongezeke, hivyo kwa mafunzo haya tunaamini tutakwenda kufanya mabadiliko makubwa” ameeleza Lemomo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo Naibu Mthibiti Mkuu wa shule kutoka halmashauri ya Arusha Mwalimu Donald Kabuta, ameeleza kwamba mafunzo waliyoyapata yatawanufaisha pia waliobaki ofisini, lengo ni kwenda pamoja katika kutekeleza mkakati huo.
“Wazazi bado hawana elimu kuhusu masomo ya amali, lakini kadri siku zinavyokwenda wataelewa umuhimu wake na kuuunga mkono juhudi za serikali” ameeleza Kabuta.