Na Ashrack Miraji,JamhuriMedia, Tanga

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema kuwa wanajiosayansi ni nguzo muhimu katika kufanikisha dhana ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri.

Mbibo ameyasema hayo Desemba 04, 2024 Jijini Tanga wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wanajiosayansi kwa niaba ya Waziri wa Madini.

Ndugu Mbibo amesema kuwa Wizara ya Madini inatambua nafasi na mchango wa wanajiosayansi katika Vision 2030 hivyo itaendelea kuwatumia kikamilifu ili kuwezesha utekelezaji wa dhana hii.

“Katika kufanikisha Vision 2030, wanajiosayansi wameendelea kutumia utaalamu wao katika kufanya utafiti wa kina wa kijiofizikia kwa kutumia teknolojia za kisasa kwa lengo la kutambua tabia za miamba. Utambuzi huu utawezesha kufanyika kwa tafiti nyingine za jiosayansi zenye kuwezesha kubaini aina mbalimbali za madini yapatikanayo nchini ” alieleza Mbibo.

Mbibo, kwa niaba ya Wizara ya Madini, aliwashukuru wanajiosayansi kwa utayari wao wa kubeba maono ya Vision 2030 na kutoa msaada wa kitaalamu katika kufikia utekelezaji wake.

Kupitia dhana ya Vision 2030, Wizara ya Madini inalenga kufanya tafiti za kina kwa angalau asilimia 50 kufikia asilimia 2030, ukilinganisha na sasa ambako ni asilimia 16 pekee ndiyo imefanyiwa utafiti wa kina kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wanajiolojia Tanzania, Dkt. Elisante Mshiu, alisema kuwa mkutano huo unalenga kujadili mabadiliko katika sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na mpito kutoka kwa nishati chafuzi kwenda kwenye nishati salama, ambayo ni sehemu ya malengo ya serikali.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wanajiosayansi Tanzania 2024. Mkutano huo wa siku tatu umefunguliwa leo Desemba 04, 2024 na utahitimishwa Desemba 06, 2024.

Dkt. Mshiu alisisitiza kuwa bila kuwa na Bodi ya Usajili ya Wanajiosayansi, maono ya 2030 yanaweza kukutana na changamoto kubwa. Alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa juhudi za uundwaji wa bodi hiyo zinafanyika kwa haraka ili kuendana na kasi ya maendeleo ya nchi.

Rais wa Jumuhiya ya Wanajioloji Tanzania Dkt Elisante Mshiu akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa mkutano huu unalenga kujadili mabadiliko katika sekta ya nishati.

“Kupitia Wizara ya Madini, juhudi kubwa zinafanyika na hatua hizo ziko karibu kumalizika. Tumesisitiza umuhimu wa kuharakisha mchakato huu ili kuhakikisha maendeleo yanakua kwa kasi inayohitajika,” alisisitiza Rais Mshiu.

Wanajiosayansi kutoka ndani na nje ya Tanzania walikusanyika jijini Tanga kwa mkutano wa TGS 2024, ambao unalenga kupeana taarifa za kitaalamu, kubadilishana uzoefu, na kujadili masuala yanayohusu utafutaji na uendeshaji wa rasilimali za madini, mafuta, gesi asilia, maji, na joto la ardhi.