Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

JESHI la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu saba wakiwemo askari watatu wa Hifadhi za Misitu (TFS) na mgambo wanne baada ya kusababisha kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka 4 na kujeruhi mtu mmoja kwa risasi

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo jana mbele ya waandishi wa habari.

Alisema kuwa tukio hilo limetokea Desemba 2 mwaka huu katika Kijiji Cha Igwisi Tarafa ya Kazaroho Wilaya ya Kaliua.

Alisema kuwa siku hiyo majira ya saa 8 mchana Askari wa TFS wakiwa Doria katika Hifadhi ya Msitu wa Taifa Kigosi Moyowosi walikamata trekta lenye namba za usajili T 689 DCA Mali ya Sandu Kate lililokuwa linalima ndani ya hifadhi hiyo.

Alifafanua kuwa wakiwa njiani kurudi kambini maeneo ya Igombambili kitongoji Cha Mpanda Mlowoka wananchi walijikusanya na kuzuia sskari hao wasipeleka trekta hilo kambini.

Askari hao wakiwa na silaha 2 aina ya AK 47 walifyatua risasi na kusababisha kifo cha mtoto huyo Grace Mussa (4) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya awali katika shule ya msingi Kalemela na kumjeruhi Zengo Sandu (47) ambapo risasi ilipenya chini ya kitovu na mkono wake wa kushoto.

Kamanda alibainisha kuwa uchunguzi wa daktari unaeleza kuwa chanzo cha kifo hicho ni kuvuja damu nyingi mtoto huyo .