Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas akisema hali ya Gaza ni ya kutisha na janga kubwa ambalo ulimwengu hauwezi kuendelea kupuuza.
Kauli ya Guterres ilitolewa katika hotuba iliyosomwa na naibu wake katika mkutano wa Cairo unaolenga kuharakisha misaada ya kibinaadamu kwa Ukanda wa Gaza.
Kabla ya kuelekea kwenye mkutano huo, Waziri wa maendeleo ya kimataifa wa Uingereza Anneliese Dodds, amesema nchi yake itatoa nyongeza ya dola milioni 24 kama msaada wa kibinadamu kwa Gaza na kuitolea wito Israel kurahisisha usafirishaji wa misaada.
Hayo yakiarifiwa, Shirika la Kimataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limetangaza kusitisha utoaji wa misaada kupitia kivuko muhimu kati ya Israel na Gaza cha Kerem Shalom kutokana na hofu ya usalama.
Mkuu wa Shirika hilo Philippe Lazzarini amesema kivuko hicho kimekuwa si salama kutokana na misafara ya misaada kushambuliwa na magenge ya watu wenye silaha.