Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimetoa sababu nne ambazo zimefanya Watanzania kuendelea kukiamini na kuchagua wagombea wa Chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na miongoni mwasababu ambazo zimefanya washindi ni uwepo wa migogoro katika vyama vya ipi upinzani.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Katibu wa Halmashauri Kuu(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi,Uenezi na Mafunzo CPA Amoss Makalla amesema wamekuwa katika kampeni kwa siku saba kuanzia Novemba 20 mpaka Novemba 26 na Novemba 27 uchaguzi umefanyika na kupiga kura.
“Ahadi yetu wakati wa kampeni ni kwamba CCM imeongozwa na 4R za Rais Samia Samia Suluhu Hassan za uvumilivu, ustahimili, kuheshimiana lakini pia kuhakikisha tunaendelea kujenga nchi yetu.CCM imeonesha kuheshimu kwa kufanya kampeni za kistaarab, kuheshimu ratiba wakati wa kampeni,”amesema.
Akitaja sababu za Chama hicho kushinda katika uchaguzi huo wa Serikali wa Serikali za mitaa ni kwamba wanaamini wamepewa imani hiyo ambayo wamepewa CCM imetokana na sababu mbalimbali na sababu ya kwanza wananchi wameridhika na utekelezaji mzuri wa Ilani ,miradi ya maendeleo, utatuzi wa kero mbalimbali.
“Hii imejenga imani kwa Watanzania kukiamini Chama Cha Mapinduzi lakini kikubwa miradi mbalimbali inayotekelezwa iko katika mitaa,Vitongoji,vijiji, kwa hiyo tunaamini mafanikio yaliyopatikana yalijenga imani kwa wananachi.”
CPA Makalla amesema sababu ya pili ni maandalizi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa walijua kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za mitaa , hivyo walifanya na maandalizi ya kutosha kwa kuanza kwa kufanya tathimini ya viongozi waliopo katika mitaa , vijiji na vitongoji.
“Kwahiyo kila eneo kila wilaya tuliwafanyia tathimini viongozi walioko madarakani lakini na kutambua changamoto na maoni ya wananchi.CCM haikukosea kuteua wagombea safi ambao wabakubalika na hiyo imekuwa siri ya ushindi lakini nyie ni mashuhuda kuanzia ngazi ya kitaifa mpaka ngazi ya Mashina uchaguzi huu tuliuchukulia kwa uzito mkubwa , hivyo maandalizi ya kuandaa wananchi yalikuwa makubwa na tunaamini tulikuwa na maandalizi mazuri.”
CPA Makalla amesema hatarajii mtu akaja akahoji CCM imeshindaje kwani Watanzania ni mashuhuda vyama vingine havikuwa na maandalizi,vyama vingine havijaonekana kwa wananchi miezi Saba ,wengine wamewekeza katika maandamano .
“Unafanya maandalizi kwa siku tatu unatarajia unaweza kushinda? CCM imefanya maandalizi ya kutosha kupitia viongozi wake.Changamoto ambayo wapinzani wameipata ni kutokana na kutakuwa na maandalizi ya uchaguzi.Tusitafute sababu yoyote.Sababu hakukuwa na maandalizi.”
Pia amesema sababu ya Tatu CCM imefanya kampeni zake kisayansi kuanzia uzinduzi ,kufunga kampeni pamoja uratibu na ushirikishwaji kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya shina.
Sababu ya nne iliyowafanya CCM kushinda,CPA Makalla amesema imechangiwa vizuri na migogoro ya vyama vya siasa na kuelez adui yako muombee njaa.Kwahiyo katika vyama vya siasa migogoro imefanya CCM kushinda ingawa kuna sababu nyingine nyingi.
Ametumia nafasi hiyo kuvitaka vyama vya upinzani kuendelea kuvumiliana na kujiepusha na migogoro kwani Chama chenye Mgogoro ni ngumu kushinda katika uchaguzi akitolea mfano CHADEMA ambayo kwa sasa kuna Mgogoro mkubwa na wameshuhudia Arusha wanachama wakivurugana na kupigana wakati wakielekea uchaguzi wa Serikali za mitaa.
“Najua vyama vya upinzani leo vinaongea lakini watakachoweza ni kutoa propaganda tu kwa kuituhumu TAMISEMI na CCM lakini ukweli wameshindwa uchaguzi kwasababu ya kutakuwa na maandalizi na migogoro kwa viongozi wao.Mengine yote watakayosema hayana ukweli.”