Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, imemwachia huru aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Simiyu, Dkt. Yahaya Ismail Nawanda baada ya kukutwa hana hatia.

ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alimwingilia kinyume na maumbile mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine jiji Mwanza.

Katika uamuzi kwenye kesi hiyo ya jinai namba 1883/ 2024, yenye kosa la kulawiti, ulisomwa na Hakimu, Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Erick Marley.

Katika uamuzi huo ,Hakimu Marley amesema mahakama hiyo baada ya kupitia maelekezo ya ushahidi na vielelezo imejiridhisha kuwa hakukuwa na muunganiko wa ushahidi unaoweza kumtia mshtakiwa Dk Nawanda hatiani na hivyo kumwachia huru.

Awali Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Juni, 02, 2024, majira ya saa 20:30 katika maegesho ya magari ya baa, maarufu iitwayo THE CASK iliyopo jijini Mwanza, ambapo alimwingilia kinyume na maumbile mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21, jina linahifadhiwa aliyekuwa akisoma Shahada ya Kwanza ya Ugavi na manunuzi katika chuo hicho.

Ilidaiwa pia Juni, 03, 2024, majira ya saa 11.00 katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alifika binti huyo akiomba kuonana na wahusika wanaoshughulika na haki za binadamu.

Waliomsikiliza katika jengo hilo walimshauri aende kituo cha Polisi Dawati la jinsia na watoto, ndipo alifika katika dawati hilo ngazi ya mkoa na kutoa malalamiko yake.

Alidai kuwa mtuhumiwa huyo baada ya tukio hilo la kikatili mlalamikaji alidai alimtaka afike katika baa ya THE CASK kwa ajili ya mazungumzo lakini alipofika katika eneo hilo ndipo alielekezwa kuingia ndani ya gari aina ya Toyota Crown nyeupe ambayo hakuweza kuitambua namba za usajili.

Mwanafunzi huyo wa kike aliliambia Jeshi la Polisi kuwa alipoingia kwenye gari alimkuta mtuhumiwa akiwa ameketi kwenye kiti cha dereva na kuanza mazungumzo.

Mlalamikaji baada ya tukio hilo alielekea Malimbe katika hosteli ya wanafunzi wa Chuo cha SAUT iitwayo South Village ambapo alivua nguo alizozivaa siku hiyo na kuziweka katika kapu la nguo chafu kisha kulala huku akisikia maumivu makali mwilini mwake na kuamua kumpa taarifa mama yake mzazi kwa kumpigia simu namba zinahifadhiwa.

Taarifa zinasema mama yake mzazi alimshauri akatoe taarifa hizo kwenye vyombo vya kisheria ili hatua ziweze kuchukuliwa, ndipo mlalamikaji alichukua uamuzi wa kutoa taarifa hizo katika dawati la jinsia na watoto mkoani humo ambapo alitoa maelezo yake kwa maandishi kisha kupelekwa Hospitali ya SEKOUTOURE kwa uchunguzi wa kitaalam.

Taarifa zinasema kuwa awali mtuhumiwa huyo aliwahi tena kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo Januari, 20, 2024 majira ya saa 20: 30 katika Bar ya THE CASK alipokutana nae kwa mara ya kwanza katika sherehe ya kuzaliwa ya mtu mmoja jina linahifadhiwa ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa ni mgeni mwalikwa kwenye sherehe hiyo.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa na mlalamikaji walitambulishana na kupeana namba za simu kwa ajili ya kuwasiliana kwa simu. Katika mazungumzo yao wakiwa ndani ya gari la mtuhumiwa, mwanaume huyo alimsihi akubali kufanya nae mapenzi kinyume na maumbile lakini mlalamikaji alidai kuwa hajawahi kufanya kitendo cha aina hiyo.

Inaelezwa kuwa mtuhumiwa alizidi kumbembeleza na kumshawishi kuwa asiogope kwani kwa mara ya kwanza atasikia maumivu lakini baadae atazoea na kuahidi kumbadilishia hali ya maisha yake kiuchumi kwa kumpatia 500,000 kila mwezi na kumsaidia dada yake jina linahifadhiwa kupata ajira.

Ilidaiwa kuwa wakati wanaendelea kuongea ndipo mtuhumiwa huyo alimfunua sketi na nguo za ndani kisha kumlawiti huku akimtishia kuwa asihangaike kupiga kelele kwa sababu gari lake linafahamika na kuna walinzi wamelizunguka hivyo hawezi kupata msaada wowote.

Baada ya tukio hilo mwanaume huyo alifungua mlango wa gari na mlalamikaji aliondoka. Mlalamikaji na mtuhumiwa waliendelea kuwasiliana kwa simu, Whatssap, jumbe fupi, video calls huku mtuhumiwa akimtumia fedha za kujikimu.

Ilidaiwa kuwa Februari 2024, mlalamikaji alidai siku hiyo ilikuwa ziara ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan mkoani Mwanza, ambapo mtuhumiwa alifika Mwanza na kumpigia simu mlalamikaji na wakakutana hoteli ya RYNANS BAY.

Mtuhumiwa alimtaka mlalamikaji kuwa anataka kuwa anafanya nae mapenzi kinyume cha maumbile. Mlalamikaji alidai alikataa kata kata na kwa hasira aliondoka chumbani bila maelewano.

Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa aliendelea kumbembeleza mmlalamikaji ili siku moja amkubalie ombi lake na ilipofika Juni, 02, 2024, ndipo mtuhumiwa alizidi kumbembeleza mmalamikaji wakutane ili waongee zaidi kuhusu jambo hilo.

Mlalamikaji aliamua kwenda Bar ya THE CASK akidhani mtuhumiwa alibadili nia yake, pengine anataka kuomba msamaha kwa kitendo cha kumuomba mapenzi kinyume na maumbile. Alipoingia kwenye gari ndipo alifanya tukio la ulawiti.

Dawati la jinsia na watoto mkoani Mwanza lilianza uchunguzi wa tukio hilo na kumuhoji mmlalamikaji na kumpeleka hospitali ya SEKOUTOURE kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalam baada ya kupata PF3.

Katika taarifa ya kitaalam iliyotolewa na Daktari wa hospitali hiyo jina linahifadhiwa, ameeleza kuwa katika uchunguzi wake amebaini kuwa mmalamikaji ameingiliwa kinyume na maumbile kwa kuingiziwa kitu butu katika sehemu yake ya haja kubwa na hivyo kusababisha michubuano na maumivu.

Wataalam wa uchunguzi wa kisayansi Juni, 03, 2024 walifika katika chumba anachoishi mmlamikaji na kufanikiwa kupata nguo ambazo mmlalamikaji alizivaa siku ya tukio na vielelezo vingine ambavyo vinapelekwa kwa mkemia wa serikali Kanda ya Ziwa kwa uchunguzi zaidi.

Pia mmlalamikaji alichukuliwa sampuli ya mate yake kwa ajili ya uchunguzi wa DNA huku wakisubiri mtuhumiwa atakapokamatwa aweze pia kuchukuliwa vipimo hivyo kwa hatua zaidi za upelelezi.

Baada ya mahakama kusikiliza shauri hilo imebaini mtuhumiwa hana hatia.