Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema mashambulizi makali ya angani yaliyoilenga miundombinu ya nishati ya Ukraine yalikuwa jibu kwa Kyiv kuyapiga maeneo ya Urusi kwa kutumia makombora iliyopewa na nchi za Magharibi.
Akiahidi kuwa Moscow siku zote itajibu matumizi ya Ukraine ya makombora ya ATACMS yanayotolewa na Marekani, Putin alisema jeshi lake linafikiria kushambulia kitovu cha mji mkuu Kyiv kulipiza kisasi mashambulizi yoyote ya usoni.
Wizara ya Ulinzi na Mkuu wa jeshi la Urusi wanayachagua maeneo ya kupiga na kuharibu nchini Ukraine. Inaweza kuwa vituo vya kijeshi, nyenzo za ulinzi au vituo vya kufanya maamuzi huko Kyiv. Aidha, utawala wa Kyiv umejaribu mara kwa mara kuzipiga sehemu zenye umuhimu wa kitaifa nchini Urusi: St. Petersburg na Moscow. Na majaribio haya yanaendelea.
Putin aliyasema hayo wakati wa ziara yake nchini Kazakhstan saa chache baada ya shambulizi hilo. Moscow ilirusha zaidi ya makombora 200 na droni yaliyoilenga gridi ya umeme ya Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amedai kuwa “mabomu ya kutawanyika” yalirushwa katika kile alichokiita “kuongezeka kwa kuchukiza kwa mgogoro” ambao umedumu kwa miaka mitatu sasa. Mashambulizi hayo yaliwaacha Waukraine milioni moja bila ya umeme.