Mapema mwezi huu nimejikuta nikiingia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Hii si mara yangu ya kwanza kufika katika hospitali hii kubwa kuliko zote nchini mwetu.

Kwanza, naipongeza Serikali na uongozi wa MNH kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya. Usafi ni wa hali ya juu. Majengo mapya yanajengwa kila uchao. Tabia za wahudumu si kama zile zilizoipamba Muhimbili miaka kadhaa iliyopita.

Kwa mara ya kwanza nimeshuhudia wauguzi wakikataa kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa na ndugu zao. Nimewaona wauguzi wa Sewa Haji Wodi 22 wakionyesha ujasiri huu. Yawezekana wakawapo wauguzi wachache wasiozingatia maadili, lakini kwa jumla hatuwezi kuwaunganisha wote kwenye dhambi ya kuomba na kupokea rushwa. Wakati mwingine kuwapongeza watumishi hawa kunaweza kuwapa moyo na ujasiri wa kuwahudumia wananchi vizuri zaidi.

Kwa mara ya kwanza nilimwona muuguzi akishawishiwa kupewa rushwa na ndugu wa mgonjwa, lakini akakataa kwa nguvu na kwa sauti ya juu. Kwa kuliona hilo, nikaamini kuwa kumbe tatizo si kwa wauguzi na madaktari wetu, bali ni kwa wagonjwa na ndugu zao wanaoamini kuwa hawawezi kuhudumiwa bila kutoa rushwa.

Nawapongeza wahudumu wa mapokezi katika Hospitali ya Muhimbili kwa namna wanavyowapokea wagonjwa, ndugu wa wagonjwa na kuwahudumia kwa lugha ya unyenyekevu na staha. Lakini hii haina maana kwamba mambo yameshakuwa mazuri kwa asilimia mia, la hasha. Bado wapo watumishi walioapa kuomba na kupokea rushwa bila kujali kuwa wateja wao wengi ni makabwela.

Pamoja na pongezi hizo, nawasihi sana Muhimbili waendelee kulinda hadhi ya majengo, hasa pale mapokezi ambako tayari viti na viyoyozi vimeshaharibika. Uongozi ujitahidi kurekebisha mambo kabla hayajaharibika sana.

Baada ya kusema hayo, napenda kueleza jambo lililonikosesha raha kwa siku kadhaa sasa. Nilipoingia katika Wodi 22 niliwakuta kina mama wengi makabwela wanaotabika kwa maumivu makali. Baadhi yao wamekuwapo wodini kwa miezi zaidi ya miwili wakikabiliwa na maradhi mbalimbali – wamevimba miguu, wana maumivu katika uzazi, wameishiwa damu, wamepoteza matumaini ya kuishi, huku baadhi yao wanadhaniwa kwamba wanasumbuliwa na saratani ya kizazi, na kadhalika.

Wapo waliotoka mikoani kwenda kupata tiba katika hospitali hiyo. Pamoja na matatizo yao kubainishwa huko walikotoka, kitaaluma wanapaswa kupimwa tena ili wataalamu wajiridhishe na kujua ni tiba ya aina gani, na kwa hospitali gani wanastahili kupelekwa kupata matibabu.

Kina mama wengi waliolazwa Wodi 22 inasemekana wana matatizo ya saratani. Kama nilivyosema, ili waweze kupelekwa sehemu husika kwa ajili ya tiba, wanatakiwa wapimwe kwanza. Mara kadhaa vipimo vya maradhi hayo vinapatikana nje ya Muhimbili.

Mimi pamoja na ndugu zangu tulitakiwa tupeleke vipimo vya mgonjwa wetu katika hospitali iliyopo Mikocheni. Gharama ya vipimo ni Sh 40,000. Majibu ya vipimo tuliyapata baada ya siku 14. Tulipopata majibu hayo, madaktari wakaamua mgonjwa wetu akatibiwe Hospitali ya Ocean Road. Kutokana na uongozi mzuri, likaandaliwa gari la wagonjwa lililomsafirisha mgonjwa hadi Ocean Road.

Wakati mgonjwa wetu akijiandaa kupelekwa Ocean Road, mgonjwa mwingine – mama wa makamo – aliingia ndani ya gari la wagonjwa akiwa tayari naye kupelekwa Ocean Road! Kwa maneno mengine “ajifanya” kuwa ndiye mlengwa akikusudia apelekwe Ocean Road akatibiwe.

Baada ya wauguzi kumwuliza jina na kubaini kuwa si yeye aliyekusudiwa kupelekwa huko, alitakiwa atelemke. Yule mama mgonjwa alilia sana. Aliangua kilio kwa namna ambayo kila aliyekuwa karibu alilengwalengwa na machozi. Kila aliyemwona alimhurumia kwa maneno ya kulalamika aliyokuwa akiyatoa huku yakiambatana na machozi. Alilia kwa sababu amekosa fursa ya kutibiwa kwa miezi zaidi ya miwili sasa. Muda wote amekuwa wodini.

Ndugu na jamaa zake hawana uwezo wa kifedha wa kugharimia Sh 40,000 ili akapimwe katika hospitali binafsi kabla ya kupelekwa Ocean Road. Wauguzi wakamwambia hawezi kupelekwa Ocean Road hadi ndugu zake watoe fedha za vipimo. Kusikia hivyo, yule mama alilia sana akisema hana ndugu wa kumsaidia.

Huyu mama ni mmoja kati ya kina mama wengi waliolazwa Wodi 22 waliokata tamaa ya kuishi. Wanaangua vilio usiku na mchana wakiomba roho zao zitoke ili waachane na maumivu makali yanayowasibu.

Ndugu zangu, kama kuna watu wenye uwezo, taasisi, mashirika na yeyote awaye, wazuru Wodi 22 wajionee namna Watanzania wenzetu wanavyotabika. Mama zetu wanatabika kwa sababu hawana Sh 40,000 za kuwawezesha kupimwa na hatimaye kupata matibabu Ocean Road!

Wauguzi na madaktari wanaweza kuwa na nia nzuri ya kuwasaidia wagonjwa hawa, lakini wanakwazwa na vipimo vinavyohitaji fedha. Hawa hawawezi kupata fedha za kuwasaidia Watanzania hawa.

Ndugu zangu, tumekuwa makini sana kuchangia harusi. Tumekuwa makini sana kuchanga kwenye misiba. Tujitahidi basi kuwasaidia ndugu zetu hawa wanaotabika ili wapone, badala ya kusubiri kununua majeneza na kuandaa vyakula na vinywaji vya kila aina wakati wa misiba. Uungwana huu uonyeshwe wakati wa ugonjwa.

Tunaweza kuamua kuwa kwenye michango ya harusi, asilimia japo moja tuwe tunaichanga kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa na watu wenye mahitaji maalumu. Nimeutoa mfano wa wagonjwa hawa kina mama katika Wodi 22 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini ukweli ni kwamba hawa ni tone tu katika bahari ya wagonjwa wanaotabika sehemu mbalimbali katika taifa letu.

Kuna wagonjwa wengi sana wanaougulia majumbani kwa kukosa fedha za matibabu. Wengi wanakufa kwa magonjwa yanayoweza kutibika, lakini wanakufa kwa sababu tu ya umasikini. Ndugu zangu kina mama, miongoni mwenu mpo wasomi ambao mna ukwasi na ushawishi wa kutafuta misaada kwa ajili ya kuwasaidia kina mama wenzenu katika Wodi 22 na kwingineko. Jitokezeni sasa muwasaidie.

Kina baba, bila kina mama ninyi hampo. Kina mama ni wazazi wenu. Kaeni mjitafakari muone ni kwa namna gani mnaweza kupunguza maumivu ya mama zenu hawa. Hali kadhalika kwa vijana; hawa ni wazazi wetu. Ni jambo la kuumiza sana kuwashuhudia mama zetu wakitabika ilhali tukitambua kuwa tunao uwezo wa kuwasaidia.

Najua kuna kisingizio cha ugumu wa maisha. Ni kweli, lakini hakuna wakati ambao maisha yamekuwa mepesi. Tunaweza kusubiri hadi mwisho wa dunia tusione urahisi huo. Jitokezeni sasa kuwasaidia mama zenu hawa.

Viongozi wa kidini ambao wana ukwasi mkubwa kutokana na makanisa na misikiti yao mikubwa kuvuta waumini wengi, nao wana kila sababu ya kuzuru katika maeneo haya ya hospitali kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa. Kampuni za simu zinavuna mabilioni ya shilingi kutoka kwa wateja wakiwamo wagonjwa! Zijitokeze sasa kuwasaidia fedha za vipimo ili waweze kutibiwa.

Kwa uongozi wa Hospitali ya Muhimbili nina ombi moja. Ianzishe utaratibu wake kupitia kitengo cha uhusiano, wa kuwatambua wagonjwa wenye mahitaji maalumu na kisha kutoa taarifa zao katika vyombo vya habari. Kama kweli mgonjwa anaweza kulazwa kwa miezi mitatu akiwa amekosa Sh 40,000 za vipimo, huyo hadanganyi. Anastahili msaada. Hospitali walimolazwa ndizo za kwanza kuwatambua.

Mwisho, wananchi wote tushirikiane kupiga vita wale wote wanaotafuna fedha za umma. Hao ni chanzo cha kuwapo matatizo ya ukosefu wa fedha ambao matokeo yake ni kukosekana kwa huduma za tiba. Kama hospitali binafsi inaweza kuwa na mashine za kupima ugonjwa, lakini Muhimbili ikakosa mashine hiyo, ni lazima tujue tuna tatizo kubwa kitaifa.

Nihitimishe kwa kuwaomba wasamaria wote kutembelea Wodi 22 kwa ajili ya kuona namna ya kuwasaidia kina mama makabwela wanaotabika na kufa kwa kukosa Sh 40,000 za vipimo!

Mungu awabariki sana.