Takribani watu 30 wanahofiwa kufa baada ya kutokea maporomoko ya ardhi katika kijiji kimoja mashariki mwa Uganda. Hayo yamesemwa na afisa mmoja wa eneo hilo aliyeonya kuwa idadi hiyo huenda ikapanda.

Mkuu wa Wilaya ya Bulambuli, Faheera Mpalanyi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa maporomoko ya ardhi yalitokea katika kijiji cha Masugu na kuwa miili sita, ukiwemo wa mtoto mdogo, imepatikana mpaka sasa.

Bi Mpalanyi amesema kutokana na uharibifu na ukubwa wa eneo lililoathirika na jinsi familia zilizoathirika zinavyotuambia, watu kadhaa hawajulikani waliko na kuna uwezekano wamefukiwa kwenye vifusi.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda John Cliff Wamala amesema miili 13 imepatikana. Amesema zaidi ya nyumba 40 zimeharibiwa kabisa. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda ilitoa tahadhari, ikiandika kwenye mtandao wa X kuwa mvua kubwa iliyonyesha jana Jumatano katika maeneo tofauti ya Uganda ilisababisha maafa katika maeneo mengi.

Taifa hilo la Afrika Mashariki limekumbwa na mvua kubwa katika siku za karibuni, huku kukishuhudiwa mafuriko kaskazini magharibi mwa nchi baada ya mkondo wa Mto Nile kuvunja kingo zake.