Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma

Polisi mkoani Kigoma imemtia mbaroni mtu mmoja anayetuhumiwa kukutwa na karatasi za kupigia kura akiwa na nia ya kuziingiza kwenye kituo cha kupigia kura ili ziingizwe kwenye boksi la kura.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma,Filemon Makungu amethibitisha kukamatwa kwa mtu huyo ambaye anashikiliwa kituo kikuu cha Lolisi mkoani Kigoma wakati tuhuma za shauri hilo likiendelea kuchunguzwa.

Kamanda Makungu alisema kuwa mtu huyo ambaye alikataa kutajwa jina alikamatwa katika eneo la Mwandiga Halmashauri ya wilaya Kigoma huku baadhi ya watu wakidaiwa kuwa na mtuhumiwa huyo alikuwa na nia ya kuziingiza kura hizi kupitia vituo vya Mgera A na B kata ya Mwandiga.  

Sambamba naye alisema kuwa Polisi ilimkamata mtu mwingine ambaye jina lake na chama anachoshabikia vimemehifadhiwa akituhumiwa kuhusika pia na kura zilizokamatwa ambapo mtu huyo alihojiwa na kuachiwa huru.

Akizungumzia suala hilo Msimamizi wa kituo cha kupigia kura cha Mgera B, Yussuf Mwita Omari alisema kuwa amesikia kuwepo kwa tuhuma hizo lakini kituo kwake hakuna tukio lolote lililotokea na kwamba jambo hilo limetokea mtaani nje na kituo hicho.

Omari alisema kuwa alishirikiana na mawakala wote wa kituo kuhakiki zoezi zima kwa mujibu wa taratibu na hadi kufikia mchana zoezi la upigaji kura lilikuwa likiendelea vizuri bila changamoto yeyote.