Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Veronica Nduva ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa uzito wa kipekee agenda ya maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo kilele chake ni tarehe 30 Novemba 2024.
Mhe. Nduva ametoa pongezi hizo wakati akitoa taarifa ya masuala mbalimbali ya kiutendaji kuhusu Sekretarieti ya EAC ikiwa ni pamoja na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya maadhimisho hayo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kutoka Nchi Wanachama kinachoendelea jijini Arusha.
Amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mkoa wa Arusha na kwa kushirikiana na Sekretarieti ya EAC imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuandaa shughuli mbalimbali kuelekea kilele cha maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kuandaa tamasha la maonesho ya barabarani, maonesho ya utamaduni na zoezi la upandaji miti.
Kuhusu matukio muhimu kwenye maadhimisho hayo, Mhe. Nduva amesema zipo program za pembezoni za Ngazi ya Juu kuhusu maadhimisho hayo zitakazowahusisha Wakuu wa Nchi wa EAC pamoja na Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Wakuu hao wa Nchi utakaofanyika tarehe 29 na 30 Novemba 2024.
Amesema patakuwa na mijadala mbalimbali yenye mada kuhusu masuala ya Biashara na Uwekezaji katika Jumuiya, masuala ya Kidigitali na Amani na Usalama pamoja na tukio la upandaji miti kama kumbukumbu nzuri ya maadhimisho hayo.
Pia ameendelea kuzihamasisha Nchi Wanachama kushiriki katika maadhimisho hayo muhimu kwao ambayo ameyataja kama moja ya kipimo cha mafanikio ya Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka
1999.
“Kama Nchi Wanachama tunajivuniamiaka 25 ya Jumuiya imara ambayo ni nusu karne, sina uhakika wengi wetu tuliopo kwenye chumba hiki tutakuwa wapi tunapoitafuta miaka mingine 25 ya Jubilee ya Jumuiya.
Hivyo, nawaomba tuungane pamoja kuanzia tarehe 29 hadi 30 Novemba 2024 kusherehekea miaka hii 25 ya mafanikio ya Jumuiya yetu”, alisema Mhe. Nduva.
Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulisainiwa jijini Arusha tarehe 30 Novemba 1999. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Tunasherehekea miaka 25 ya Mtangamanao wa Kikanda na Maendeleo”.
Mkutano wa Makatibu Wakuu wa EAC kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki umemalizika leo tarehe 26 Novemba 2024 ambapo Mkutano wa Baraza hilo utafanyika tarehe 28 Novemba 2024.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi.