Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amewataka wananchi kupiga kura za hapana katika mitaa ambayo wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamebakizwa pekee baada ya vyama vya upinzani kuenguliwa.
Zitto ametoa wito huo siku ya Jumanne Novemba 26, 2024 wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji 2024- 2029 uliofanyika katika uwanja wa Mwanga Community Centre uliopo katika kata ya Mwanga Kaskazini, Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.
“Kwahl hiyo ukiingia kwenye eneo la kupigia kura, ukakuta mtaa mgombea ni wa CCM peke yake, maelekezo ya chama ni kupiga kura ya hapana. Kura za hapana zikiwa nyingi, mitaa hiyo uchaguzi utarudiwa,” amesema Zitto huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti ushawishi wa CCM katika maeneo yenye upinzani mkubwa.
Zitto amewaambia wananchi kuwa haitakiwi mtaa wowote katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kuongozwa na CCM. Amewahimiza wapigakura kuunga mkono wagombea wa vyama vingine vya upinzani pale ambapo ACT Wazalendo haina wagombea.
“Ukifika kwenyw kituo cha kupigia kura, ukakuta hakuna mgombea wa ACT Wazalendo, angalia mgombea wa chama kingine chochote cha upinzani, mpe kura. Lengo letu mji wetu tuondokane na CCM kabisa”, ameongeza Zitto.
Zitto amefafanua kuwa uchaguzi huu wa serikali za mitaa una maana kubwa mbili kwa wakazi wa Kigoma. Kwanza, ni fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya matukio aliyoyataja kuwa ya “wizi wa kura” kwenye uchaguzi wa 2020 kwa kuwapigia kura wagombea wa upinzani. Pili, ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kuhakikisha kuwa ACT Wazalendo inakuwa na wajumbe wengi wa maendeleo ya kata (Wanaotokana na wenyeviti wa mitaa) ambao watawasaidia madiwani wa kata kama watachaguliwa mwakani kwani uchache wa wajumbe hao utawapa wakati mgumu madiwani wa ACT.
Aidha ameeleza kuwa watu wa CCM wameishiwa hoja za kuwashawishi wananchi ili waendelea kuwapa mamlaka isipokuwa kutegemea vyama vya upinzani kutotangazwa washindi ikiwa vitashinda, na kutegemea kura za bandia. Kutokana na hilo amewaambia watu wa CCM kuwa njama hizo hazitawezekana kwani ACT imejiandaa vyema kukabiliana nazo.
“Wananchi wote wa Manispaa ya Kigoma Ujiji nenda kapige kura, chukua kura yako moja, mchague unayemtaka, usithubutu kuingia na kura ya ziada, kwasababu yatakayokukuta tusilaumiane”, ameonya Zitto.