Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
IDADI ya watu waliopoteza maisha baada ya kufukiwa na jengo lililoporomoka Kariakoo jijini Dar es Salaam imefikia 29.
Jengo hilo liliporomoka mapema Jumamosi ya Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26, 2024 katika eneo hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amesema zoezi la kufukua kifusi limehitimishwa.
“Napenda kuutaarifu umma kuwa sasa tumetamatisha kazi ya kufukua kifusi kwani tumefika mwisho kabisa wa jengo lenyewe. Na mpaka kufikia mchana huu kuna wenzetu tisa wameongezeka hivyo kufikia vifo 29,” amesema Makoba.
Makoba amebainisha kuwa, zoezi linaendelea la kutambua miili kwa kutumia Teknolojia ya DNA.
“Zipo kesi zinategemea uchunguzi wa vinasaba, kulingana na hali ya ajali hivyo inabidi kutumia Teknolojia nyingine ya DNA ili kuweza kutambua baadhi ya miili, na zoezi linaendelea majibu yatakapokuwa tayari tutawafahamisha,” amesema.
Hata hivyo amesema kamati ya maafa kitaifa iliweka kambi katika eneo hilo tangu siku ya tukio, hivyo zoezi hilo kwasasa linapelekwa kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na watasimamia eneo hilo na taratibu zingine zitatangazwa.
Aidha amesema kuwa hatua itakayofuata ni Wafanyabiashara kutambua mali zao ambazo zilitolewa katika eneo hilo.
“Wafanyabiashara wanatakiwa wafahamu mali zote zilizokuwa hapa zimetolewa, na serikali imezihifadhi mahali salama kwenye maghala ziko chini ya usimamizi mzuri.
“Lengo tulikubaliana na wafanyabiashara tuzike kwanza, tuokoe ndugu zetu halafu ndo tuje kwenye suala la Mali. Lakini pia, ilikuwa ni ngumu kuanza kuambiana mali hii ya nani hivyo tukakubaliana zikusanywe sehemu moja na baada ya hii shughuli zoezi linalofuata ni kwenda kuangalia kila aliyekuwa na mali na imetoka humu ndani anaipata kihalali,” amesema Makoba.
Vilevile Makoba ametangaza kufunguliwa kwa maeneo yaliyokuwa yamefungwa ili biashara ziendelee.
“Tangu tarehe 16 sehemu nyingi za biashara zilifungwa na sababu nyingi ni usalama wa maisha na Mali za watu. Sasa kwa leo tulipofikia serikali inatangaza kuwa maeneo yote ya Kariakoo yanafunguliwa kuendelea na biashara isipokuwa Mtaa wa mchikichini unaokutana na kongo, na kipande cha mchikichini na Manyema.
“Eneo hili halitatumika kwasababu kuna taratibu za kiuchunguzi zinaendelea… bado kuna majengo mawili yaliyo karibu na jengo lililoanguka kuna wataalam waje wajiridhishe kwamba yana usalama kiasi gani na taratibu zingine za kiuchunguzi, zikikamilika watatushauri lini Barabara iendelee kutumika kama kawaida,” amesisisitiza Makoba.
Wakati huo huo, Makoba amewahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura pamoja na kudumisha amani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kuwa kupitia janga hili anaamini Wafanyabiashara wadogo (machinga) watakuwa wamejifunza kwamba kuzifunga Barabara Kwa kufanya biashara ni hatari.
“Ipo siku tunaweza tukaunguliwa vitu vyetu fire ikakosa pa kupita, hivyo ni muda muafaka wa viongozi wa Wafanyabiashara wadogo kuanza kutafakari namna sahihi ya kuzifungua njia hizi ili tunapopata majanga yoyote iwe rahisi kupita na kwenda kuokoa.
“Pia jambo lingine tumejifunza namna ya kutunza mizigo yetu, kwamba sababu una duka unaweza kutawanya mizigo sehemu nyingine ili inapotokea majanga unakuwa na mzigo mwingine,” amesema na kuongeza kuwa:
“Tumejifunza kwamba unapopanga nyumba yoyote ya biashara jambo la kwanza kuhakikisha nyumba hiyo ina bima ili yakitokea majanga bima inalipa kuanzia mwenye duka mpaka mwenye jengo,” amesema Chalamila.