Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya dola, imekamata jumla ya kilogramu 2,207.56 za dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam ambapo Watuhumiwa saba wanashikiliwa kuhusiana na dawa hizo.
Akiongea jijini Dar es Salaam leo Novemba 25, 2024, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema kati ya dawa zilizokamatwa, skanka ni kilogramu 1,500.6, methamphetamine kilogramu 687.76, heroin kilogramu 19.20, na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl.
“Novemba 14, 2024, jijini Dar es salaam, katika Wilaya ya Kigamboni, Mtaa wa Nyangwale, Watuhumiwa Mohamed Suleiman Bakar (40) na Sullesh Said Mhailoh (36), wote Wakazi wa Mabibo, Dar es salaam, walikamatwa wakiwa na kilogramu 1,350.4 za dawa za kulevya aina ya skanka, dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba aliyopanga Mohamed, ambayo aliitumia kama ghala la kuhifadhi dawa hizo, dawa nyingine zilipatikana ndani ya gari aina ya Nissan Juke yenye namba za usajii T 534 EJC, zikiwa tayari kwa kusambazwa”
“Tarehe hiyohiyo, katika Mtaa wa Pweza Sinza E, Wilaya ya Ubungo,, Iddy Mohamed Iddy (46), Mkazi wa Chanika Buyuni, alikamatwa akiwa na kilogramu 150.2 za skanka, zilizokuwa zimefichwa katika maboksi ya sabuni na baadhi ya dawa hizo zikiwa zimefichwa kwenye boksi lililotengenezwa kwa bati ngumu na kupachikwa kwenye chassis ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika Kusini LN87XJGP, ambalo limekuwa likitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nje ya Nchi”
“Vilevile, November 17, 2024, katika Jiji la Tanga, Watuhumiwa Ally Kassim Ally (52) na Fahadi Ally Kassim (36) walikamatwa mtaa wa Mwakibila wakiwa na kilogramu 706.96 za dawa aina ya heroin na methamphetamine, baadhi ya dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 714 EGX, huku nyingine zikibainika kufichwa kwenye nyumba aliyopanga Mtuhumiwa”