Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tanzania imefanikiwa kushinda tuzo ya kuwa eneo maridhawa zaidi kwa utalii wa safari duniani katika hafla ya ugawaji tuzo za utalii duniani (World Travel Awards) zilizofanyika nchini Ureno.
Tuzo za World Travel Awards (WTA) zinatambulika kama tuzo za juu zaidi duniani katika sekta ya utalii tangu mwaka 1993 .
Tuzo hizo zimekuwa zikitambua mafanikio na umahiri katika ngazi ya mabara na kidunia katika kategoria za utalii.
Tuzo hizo zimetolewa usiku wa kuamkia leo, yaani Novemba 24, 2024 kisiwani Madeira nchini Ureno.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa ushindi huo Dkt: Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii ameielezea tuzo hiyo kuwa ni sehemu ya ushahidi wa uhifadhi mkubwa uliofanywa na viongozi wa awamu zote na unaoendelezwa katika awamu ya sita chini ya Rais Dkt: Samia Suluhu Hassan.
“Tuzo hii ni ushahidi wa matokeo ya uhifadhi wetu mkubwa uliofanywa na viongozi wa awamu zote na unaoendelezwa katika Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia na uwekezaji mkubwa tunaoendelea nao katika kutangaza utalii kwani wengi walioipigia kura Tanzania maana yake ni wazi walitembelea na kuridhika na umaridhawa na uasili wa hifadhi zetu,”
Awali mwezi Oktoba mwaka huu, Tanzania ilishinda Tuzo nne za WTA katika ngazi ya Bara la Afrika ikiwemo ile ya “Africa’s Leading Destination.”
Awali katika Tuzo hizo kampuni binafsi inayofanya kazi Tanzania katika Hifadhi za Serengeti na Ruaha ya Serengeti Balloon Safaris nayo imeshinda Tuzo ya kuwa Kampuni Bora ya Baluni Duniani.
Baadhi ya nchi nyingine zilizoshinda ni Visiwa vya Saint Lucia (Honeymoon Destination), ugiriki (Athens, Leading City Destination), Ureno (World Leading Beach Destination), Ufaransa (Leading Events Destination), Peru (Cultural and Culinary Destination), Ureno (Praga, Emerging Tourism Destination), Hispania (Madrid, World Leading Meeting Destination) na Maldives (World Leading Destination).
Kwa mafanikio hayo Rais wa WTA Bw. Graham Cooke pia ameitangaza Tanzania kuwa mwenyeji wa Tuzo za Utalii Duniani Kanda ya Afrika mwaka 2025.
Hatua hiyo ya ushindi wa tuzo kwa Tanzania inatajwa kama hatua ku8bwa zaidi ya mafanikio kufikiwa na taifa katika historia ya sekta ya utalii nchini.