Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kuajiri walimu wa somo la biashara 4,000 kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Walimu hao watafuata mtaala mpya unaotumika, unaolenga kuleta mapinduzi ya elimu nchini kwa kuimarisha elimu ya biashara kwa wanafunzi.
Akifungua Mafunzo Elekezi ya siku tatu kwa Maofisa Udhibiti ubora wa Wilaya Wateule jijini hapa jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema walimu hao watafundisha elimu ya biashara kuanzia mwakani.
“Katika mageuzi ya elimu, wanafunzi wanatakiwa kusoma somo la biashara kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ili kuhakikisha wanapata elimu hiyo muhimu ya mafunzo ya biashara na ndiyo maana Rais Samia ametoa kibali kuajiri walimu hao,” alisema.
Aliongeza, “Watoto lazima waanze kuandaliwa ili kuweza kujiamulia cha kufanya baada ya kumaliza kidato cha nne kwani watakuwa wamefundishwa mbinu za biashara zitakazowasaidia katika maisha yao, hata wakifeli kuendelea na masomo wanaweza kujiajiri.”
Aliwapongeza wadhibiti ubora waliopenya kwenye mchujo akisema waliopatikana ni kwa sifa na vigezo vinavyopimika, wana shahada ya uzamili, wana uzoefu na wana maadili na uwezo wa kufanya kazi vizuri.
Aliwatia moyo wadhibiti ubora 40 waliofeli katika mchujo huo kwamba waombe kujiendeleza ili wawe na shahada ya uzamili na wizara ipo tayari kuwalipia na wakihitimu wataangaliwa.
Aliwaagiza wadhibiti ubora hao wa wilaya wateule kwenda kufanya kazi kwa bidii katika kusimamia mageuzi katika sekta ya elimu kwa sababu wao ni jicho la wizara. Alisema ndiyo maana rais amewakubali na kukubali muundo wa uwepo wao katika halmashauri zote nchini.
Pia, aliwataka wakatupie jicho kwenye tume ya watalaamu kutoka taasisi za elimu nchini ambayo inafanya kazi ya kuunganisha mifumo ya kuwatambua wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu ili ajulikane alikosoma na kazi anayofanya.
Aliwaagiza pia waangalie elimu ya msingi yatakayoanza 2027. Mkenda aliwaagiza kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri na walimu moja kwa moja kwa kuunda kundi la kuwaunganisha.
Kaimu Katibu Mkuu, Michael John aliwapongeza wadhibiti ubora 179 waliofika kwenye semina elekezi hiyo ya siku tatu na kuhakikisha wanakwenda kusimamia Sera ya Elimu 2014 toleo 2023 pamoja na utekelezaji wa mtaala mpya ambao katika maboresho ya muundo wa uwepo wao katika halmashauri zimeondolewa ofisi za kanda.