Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanian , Dkt: Samia Suluhu Hassan imeweka wazi juu ya mipango yake ya kuhakikisha sekta ya madini nchini inakuwa miongoni mwa sekta zitakazokuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Hatua hiyo imekuja wakati wa mkutano mkuu wa kimataifa wa madini uliofanyika jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Mkutano huo ulihusisha wadau na makampuni mbalimbali mbalimbali zinazojishughulisha na shughuli za madini zikiwemo uchimbaji, uchakataji, uuzwji wa vifaa vya uchimbaji pamoja na uuzwaji wa madini yenyewe.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo wa kimataifa akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt: Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameelezea juu ya mipango iliyowekwa na serikali katika kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuongeza mchango wake katika pato kuu la taifa na kufikia lengo lililowekwa na serikali la kuhakikisha sekta hiyo inachangia zaidi ya asilimia 10 katika pato la serikali mpaka kufikia mwaka 2025.
Kwa kuzingatia hilo Waziri Mkuu Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali inazidi kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kufanya mapitio ya kisera, kisheria na kikanuni pamoja na kuipitia miongozo mbalimbali ili kuweza kushughulikia hasa katika eneo la ukuaji wa thamani wa madini.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuongeza mchango wake katika pato la taifa kwa kuhakikisha sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 10 katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.”
“Serikali inazidi kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kufanya mapitio ya kisera, sheria na kanuni pamoja na miongozo mbalimbali ili kuweza kushughulikia changamoto hasa kwenye eneo la ukuaji wa thamani wa madini.”
Waziri Mkuu Majaliwa ameonesha kufurahishwa na uchangiaji wa sekta ya madini katika pato la taifa kwa siku hadi siku ambapo alitoa takwimu zilizoonesha ukuaji wa sekta hiyo kutoka asilimia 5.3 mwaka 2021 mpaka kufikia asilimia 9 kwa mwaka 2024 ambapo ameitaja kama ni hatua nzuri kwa sekta hiyo katika safari ya kufikia uchangiaji wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Aidha waziri mkuu Majaliwa ameongeza kuwa serikali imechukua hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa wawekezaji wakubwa na wadogo katika sekta ya madini wanaendesha shughuli zao kwa tija na kuwezesha mazingira wezeshi ya uwekezaji na upatikanaji wa teknolojia unaimarika.
“Hii ni pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo serikali imeamua kuimarisha kwa lengo la kuvutia uwekezaji na kuwezesha uwekezaji huo kuweza kufanyika kwa kila mwekezaji.”
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyopangwa kutekelezwa na serikali katika kutengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika sekta hiyo nchini Waziri Majaliwa ameyataja maeneo mbalimbali kama kuongeza uwezo wa nishati ya umeme kwenye gridi ya taifa pamoja na uimarishwaji wa njia za usafirishaji.
Waziri Majaliwa pia amegusia juu ya suala la vituo vya madini ambapo mipango ya serikali iliyopo ni kuviongezea uwezo ambapo kwa kulitambua hilo serikali imeshafanya kazi kubwa ya kusogeza vituo katika kila mkoa na mpaka sasa kuna jumla ya masoko 44 katika mikoa mbalimbali nchini na vituo 103 vya kunolea madini.
“Kupitia masoko na vituo hivyo kumekuwa na mfumuko mzuri wa ukusanyaji wa ukusanyaji wa madini hasa kwa mwaka 2023/24” Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Nae Waziri wa madini, Anthony Mavunde kupitia mkutano huo ameelezea baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa na sekta hiyo ambapo katika dhamira ya serikali katika kukuza sekta ya madini kumekuwa na ongezeko la bajeti kwa sekta hiyo kutoka shillingi billioni 89 mpaka shillingi billioni 231 huku akiweka wazi fedha hizo zilizozidi zimeelekezwa katika tume ya utafiti wa madini na jeolojia(GST), ambapo fedha hizo zitasaidia ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa hatua inayotajwa kuwa ni ukombozi kwa wachimbaji wadogo na wakubwa nchini.
Aidha pia Waziri Mavunde ameongeza kwa kuielezea hatua nzuri iliyofikiwa na sekta ya madini ambapo ametoa takwimu zinazoeleza kuwa kwa ya mwaka wa fedha wa 2024/25 ndani ya siku 135 sekta ya madini imeingiza shillingi billioni 392 katika pato kuu la serikali huku lengo ni kuingiza shillingi trillioni 1 ifikapo mwakani mwezi juni mwakani.
Kwa upande mwingine miongoni mwa wadau walioshiriki katika mkutano huo wa kimataifa wa madini, Ni kampuni ya uchimbaji madini ya PMM mining inayopatikana katika wilaya ya Handeni eneo la magambazi ambayo kupitia, Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo mhandisi Ulimbakisa Spendi akizungumza na gazeti la Jamhuri amepongeza hatua kubwa zilizochukuliwa na serikali kwa wachimbaji madini ikiwemo kushushwa kwa punguzo la kodi kwa makampuni kutoka asilimia 6 mpaka asilimia 4 huku akibainisha kuwa kwa hatua hizo za makusudi zinazochukuliwa na serikali ni sahihi kwa manufaa ya taifa kwani faida zipatikanazo katika madini zitabaki nchini na kuyanufaisha makampuni ya Kitanzania.