Naibu Rais aliyetimuliwa madarakani nchini Kenya Rigathi Gachagua amedokeza kurejea kwa kishindo kisiasa Januari 2025 baada ya kufanya mashauriano na wakazi wa eneo la Mlima Kenya.
Akizungumza wakati wa ibada ya kanisa mjini Murang’a siku ya Jumapili, Gachagua amesema kuwa mgogoro wake na Rais William Ruto umemruhusu kupanga upya mikakati yake ijayo ya kisiasa.
Kulingana na The Citizen Digital , Naibu huyo wa zamani alisema kwamba alibaini rasmi Rais Ruto ni mtu wa aina gani ilipodhihirika kwamba ndiye aliyechangia kuondolewa kwake na kwamba atafanya maamuzi ya busara wakati atakaporejea katika siasa.
“Sisi kama watu wa Mlima Kenya tunachukia mambo mawili; uongo na usaliti. Januari hii ijayo baada ya mazungumzo tutatoa mwelekeo wetu..
Hatutajikuta tena kwenye shimo tulimo,” alisema Gachagua.
“Rais Ruto, rafiki yangu, alifanya jambo jema kuleta vita hivi dhidi yangu na watu wa mlimani kwa sababu sasa tunamjua.
Sasa tumekuelewa (Ruto) na tutakuhutubia jinsi tunavyokujua wewe ni nani. Sasa tutakuwa na mazungumzo kwa heshima.”
Gachagua alisema kuwa amekuwa akifanya mazungumzo na viongozi wa makanisa, wafanyabiashara, wataalamu na viongozi wenye nia moja “wanaopenda watu wetu”.